Na Mwandishi Maalumu - Dodoma
Wananchi wa mkoa wa Dodoma na mikoa jirani wametakiwa kutumia maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kufanya uchunguzi wa afya na kuzijua namba zao ili waweze kuwa salama na kujilinda na magonjwa yasiyoambukiza.
Rai hiyo imetolewa na Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Daud Gwilenza wakati wa maonesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park vilivyopo jijini Dodoma.
Dkt. Daud alisema JKCI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya inafanya kampeni ya Jua Namba Zako ikiwa na lengo la kupunguza magonjwa yasiyoambukiza katika jamii kwa kuifanyia jamii uchunguzi wa afya wa mapema na kuwapa elimu ambayo itawalinda na magonjwa yanayoweza kuepukika.
“Ni jukumu letu kuhakikisha kuwa jamii inakuwa salama na inasaidiwa ili iweze kuyafahamu magonjwa yasiyoambukiza, kufahamu namna ya kujikinga na magonjwa hayo lakini pia kwa wale ambao tayari wamepata magonjwa hayo tunawapa nafasi ya kufuatilia afya zao ili wasipate madhara zaidi”, alisema Dkt. Daud
Dkt. Daud alisema kuwa watu wengi wamekuwa wakiogopa kufanya uchunguzi wa afya kwa kuhofia kuwa wakikutwa na magonjwa yasiyoambukiza watapata mtikisiko na kupoteza muelekeo jambo ambalo si la kweli kwani mtu anapogundulika mapema inamsaidia kujua namna ya kuishi, vitu vya kuacha na nini cha kufanya ili asipate madhara zaidi.
Kwa upande wao wananchi waliopata huduma katika banda la Taasisi hiyo wameipongeza JKCI kwa kuendelea kusogeza huduma hizo karibu na wananchi na kuwapunguzia adha ya kuzifuata mahali zilipo.
Dorcas Judica mkazi wa Dodoma alisema JKCI ni Taasisi ambayo ipo mstari wa mbele kuhakikisha kuwa huduma inazozitoa zinawafikia watanzania wote ndio maana imekuwa ikifanya kambi za matibabu katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
“Kwakweli Taasisi zote za afya zioneshe nia kama ambavyo JKCI inafanya kutufikishia huduma bingwa bobezi karibu na kutusaidia, kwani jamii yote inatamani kujijua na kuchukua hatua za haraka za kujikinga na magonjwa hayo”, alisema Dorcas.
Dorcas alisema uoga wa watu kufanya uchunguzi wa afya unasababishwa na hali duni ya maisha, watu wanakuwa na hofu wakikutwa na magonjwa kama ya moyo watawezaje kumudu gharama za matibabu lakini hawajui kuwa wangejijua mapema ingewasaidia kutotumia gharama nyingi kuyatibu.
Naye Ibrahimu Muimba alisema jamii ikiifahamu vizuri kampeni ya Jua Namba Zako na ikachukua hatua itasaidia kupunguza magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo hivyo kujenga Taifa lenye afya bora.
“Leo nimepata elimu ya umuhimu wa kufahamu shinikizo langu la damu, kiwango cha sukari kwenye damu, uwiano wangu wa urefu kwa uzito, mapigo yangu ya moyo na kiwango cha mafuta kwenye damu, yote haya kama nitajilidha nisiyapate basi nitakuwa salama na mwenye afya”, alisema Ibrahimu.






0 comments:
Post a Comment