Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe (Mb) amekutana na Balozi wa Australia nchini Tanzania anayemaliza muda wake, Mhe. Jenny Da Rin kwa madhumuni ya kumuaga.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, tarehe 1 Juni, 2026, Mhe. Dkt. Maghembe alimpongeza Balozi Jenny kwa kumaliza muda wake wa uwakilishi nchini kwa mafanikio na kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Australia.
Kwa upande wake, Balozi Jenny Da Rin aliishukuru Serikali kwa ushirikiano iliyompatia na kusisitiza umuhimu wa Watanzania kutumia fursa za elimu na semina zinazotolewa na Australia, akieleza kuwa maarifa na ujuzi unaopatikana kupitia programu hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Tanzania, hususan katika sekta ya madini.
Aidha, Balozi Jenny aliihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa Serikali ya Australia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta ya kilimo, ikiwemo tafiti, usimamizi wa rasilimali maji, kuongeza uzalishaji wa mazao na utekelezaji wa programu mbalimbali za maendeleo ya kilimo.
Vile vile, alielezea dhamira yake ya kuendeleza kuhamasisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Australia kuja kuwekeza nchini, huku akisisitiza umuhimu wa kutafuta suluhisho la baadhi ya changamoto zinazowakabili wawekezaji kwa manufaa ya nchi zote mbili.












0 comments:
Post a Comment