Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo
amempokea Ikulu jijini Dar es Salaam Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul
Kagame, aliyewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja. Rais Dkt. Samia na mwenzake, Rais Kagame wamefanya mazungumzo ya ana kwa ana, na
baadaye kuongoza mazungumzo rasmi ya uwili yaliyohusisha ujumbe wa nchi zote mbili,
na kufuatiwa na mazungumzo na waandishi wa habari.
Viongozi hao wamejadili hatua za kuimarisha ushirikiano katika biashara na uwekezaji,
uchukuzi na miundombinu, nishati, ulinzi na usalama, uhamiaji, pamoja na uratibu wa
misimamo ya nchi hizo mbili katika masuala ya kikanda na kimataifa.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Rais Dkt. Samia amesema Tanzania na
Rwanda zimeendelea kujenga uhusiano wa undugu, ujirani mwema na urafiki wa
kihistoria, unaoakisi mshikamano wa muda mrefu kati ya wananchi wa pande zote mbili.
Rais Dkt. Samia amesema biashara kati ya Tanzania na Rwanda imeendelea kukua na
kufikia thamani ya shilingi bilioni 644 mwaka 2025.
Amesema kuanzia mwaka 1990 hadi
mwezi Machi, 2026, Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania imesajili miradi 42 ya uwekezaji
kutoka Rwanda yenye thamani ya dola za Marekani milioni 325.5, iliyozalisha ajira 2,225
kwa Watanzania.
Pamoja na hatua hiyo, Rais Dkt. Samia amesema nchi zote mbili zimekubaliana kuongeza
kasi ya kuondoa changamoto za kibiashara, ikiwemo vikwazo visivyo vya kikodi, ili
kupanua biashara na uwekezaji, na kutumia kikamilifu fursa za soko la pamoja la Afrika
Mashariki na Soko Huru la Biashara la Afrika.
Katika uchukuzi na miundombinu, Rais Dkt. Samia amesema takribani asilimia 70 ya
shehena za Rwanda hupitia bandari za Tanzania, na kwamba Tanzania itaendelea kuweka
mazingira bora ya kuhudumia shehena hizo, ikiwemo huduma maalum katika bandari,
matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Tanga, pamoja na maeneo ya
kuhifadhi mizigo.
Marais hao pia wamejadili uendelezaji wa miundombinu ya reli na barabara, ikiwemo
mradi wa reli ya Isaka hadi Kigali, unaolenga kuharakisha usafirishaji wa bidhaa na
kuongeza ufanisi wa biashara kati ya nchi hizo mbili.
Katika nishati, viongozi hao wamejadili Mradi wa Umeme wa Maporomoko ya Rusumo,
unaozihusisha Tanzania, Rwanda na Burundi, wenye uwezo wa kuzalisha megawati 80,
pamoja na makubaliano ya kuuziana umeme kati ya Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) na Shirika la Umeme la Rwanda (REG), kwa ajili ya kuchochea shughuli za
kiuchumi kwa manufaa ya nchi zote mbili.
Kwa upande wake, Rais Paul Kagame amemshukuru Rais Dkt. Samia na Watanzania kwa
mapokezi mazuri, akisema Tanzania ni mshirika muhimu wa Rwanda, hususan katika
biashara na usafirishaji kupitia bandari zake zinazoiunganisha Rwanda na masoko ya
kimataifa.
Rais Kagame amesema Tanzania na Rwanda zinapaswa kuimarisha msingi imara wa
uhusiano uliopo kwa kuendeleza ushirikiano katika maeneo ya kimkakati ili kukuza
biashara, kuendeleza miradi ya pamoja na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya nchi
hizo mbili.
Aidha, amesema Rwanda itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania katika
kuimarisha ushirikiano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Afrika na
majukwaa mengine ya kimataifa, kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
Ziara ya Rais Kagame nchini inadhihirisha nafasi muhimu ya Tanzania katika biashara na
ushirikiano wa kikanda, kama mshirika wa karibu na lango la biashara kwa nchi jirani,
huku makubaliano yaliyofikiwa yakitarajiwa kuongeza biashara, kurahisisha usafirishaji
na kufungua fursa zaidi kwa wananchi wa nchi zote mbili.



.jpeg)



0 comments:
Post a Comment