Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) leo tarehe 29.04.2026 imezindua awamu ya pili ya kupokea mawazo bunifu kutoka kwa Umma katika kuongeza wigo wa kodi na kuboresha huduma za kodi nchini.
Akizindua awamu hiyo ya pili ya kupokea mawazo bunifu kutoka kwa Umma katika kuongeza wigo wa kodi na kuboresha huduma jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema lengo la kuwashirikisha wananchi kutoa mawazo yao ni kutaka maboresho yanayofanywa na TRA pamoja na ubunifu utokane na wananchi wenyewe.
Amesema TRA ni chombo cha wananchi kinachokusanya kodi kwa wananchi kwaajili ya wananchi hivyo ni hatua muhimu kuwashirikisha kutoa mawazo yao ya ubunifu ikiwa ni awamu ya pili huku awamu ya kwanza ikitajwa kuwaibua wabunifu 9 kati ya 106 waliofika kwenye hatua ya pili kutoka wabunifu 5,681 waliowasilishq mawazo yao.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema awamu ya pili ya Tuzo imeboreshwa kwa kiasi kikubwa kwa kuweka Kamati huru itayoratibu kazi zote zitakazotumwa na waombaji ambayo haihusishi watumishi wa TRA huku zawadi zitakazotolewa nazo zikiwa zimeboreshwa.
Amesema mshindi wa kwanza atajipatia Sh. Milioni 50, washindi wawili wa Pili watapata milioni 30 kila mmoja, washindi wa nafasi ya tatu wawili watapata Sh. Milioni 20 kila mmoja huku washindi wengine 15 wakipatiwa Sh. Milioni 10 kila mmoja ambapo washiriki ambao wazo lao litafika hatua ya pili watapatiwa Sh. Laki moja kwa kila mmoja wao.
Kukusu maeneo ya kipaumbele yatakayozingatiwa kwenye bunifu hizo amesema miongoni mwake ni Upanuzi wa wigo wa kodi hususan katika sekta isiyo rasmi, urahisishaji wa ukadiriaji na ulipaji wa kodi kwa wafanyabiashara wadogo, Maboresho ya huduma za Kidijitali, Maboresho ya utatuzi wa migogoro ya kikodi na matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa kodi.
Kamishna Mkuu Mwenda amewahakikishia wote wanaotarajia kuwasilisha mawazo yao ya ubunifu kuwa matarajio yao yatafikiwa hivyo wajitokeze kwa wingi kutuma mawazo bunifu.
Awali akimkaribisha Kamishna Mkuu, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mcha Hassan Mcha mawazo bunifu yatakayotolewa yanatarajiwa kuongeza ufanisi katika masuala ya kodi na kutatua baadhi ya changamoto ikizingatiwa kuwa changamoto za kodi zinahitaji ushirikishwaji na matumizi ya teknolojia katika utatuzi wake.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango Dkt. Ephraim Mdee amesema awamu hii wamefanya Maboresho makubwa kwa vigezo na zawadi zinazotolewa na hiyo ni baada ya kupata uzoefu katika awamu ya kwanza sambamba na maoni ya wadau mbalimbali.















0 comments:
Post a Comment