Nafasi Ya Matangazo

April 21, 2026










Na Mwandishi Wetu, Dodoma 
Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania (TCM) imejadili na kuweka mikakati wa kuifanya Sekta ya Madini kuwa mhimili mkuu wa kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ya kuifanya Tanzania kufikia uchumi wa thamani ya dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050, kwa kusisitiza utafiti wa madini, usimamizi madhubuti na ushirikiano na sekta binafsi kama nguzo kuu za mafanikio hayo.

Akizungumza katika kikao na Chemba ya Migodi kilichofanyika katika ukumbi wa Tume ya Madini jijini Dodoma, leo Aprili 21, 2026, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa hatua hiyo haiwezekani bila kuwekeza kwa nguvu katika utafiti wa kina wa rasilimali madini kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Ameeleza kuwa utafiti wa madini unapaswa kupewa kipaumbele kwani ndio unaofungua milango ya uwekezaji, kuongeza tija na kuhakikisha nchi inanufaika ipasavyo na rasilimali zake.

Katika kikao hicho, Waziri Mavunde amepokea changamoto, maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau wa Sekta ya Madini kupitia TCM, akiahidi kuwa Serikali itayafanyia kazi kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wanachama wa TCM kupitisha hoja zao kupitia umoja wao ili kuwa na sauti moja yenye nguvu na kurahisisha mawasiliano kati ya Serikali na sekta binafsi.

Kwa upande wa usimamizi, Waziri Mavunde ameelekeza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini na taasisi za kiserikali ili kuhakikisha utekelezaji wa Sera na Sheria unakuwa na ufanisi zaidi bila kuingilia na kuleta usumbufu kwa wawekezaji.

Akizungumzia changamoto ya uvamizi wa maeneo yenye leseni halali za uchimbaji, Mavunde amesisitiza kuwa vitendo hivyo havitavumiliwa na tayari maelekezo yametolewa kwa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, kupitia Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuwaondoa mara moja wavamizi wote na ametumia nafasi kueleza msimamo wa serikali wa kufuta  leseni ambazo hazifanyi kazi zinazomilikiwa na wawekezaji hao.

Amefafanua kuwa Serikali inakamilisha mfumo wa kidijitali unaohakikisha kuwa leseni za utafiti zinazoisha muda wake zinarejeshwa moja kwa moja Serikalini, hatua inayolenga kudhibiti tabia ya watu kushikilia maeneo makubwa kwa matarajio ya kuvutia wawekezaji baadaye.

Katika kuimarisha ajenda ya Ushirikiwa wa Watanzania kwenye sekta ya madini, Waziri Mavunde ameeleza kuwa, kuanzishwa kwa maeneo maalum ya uwekezaji wa viwanda vinavyozalisha vifaa na vipuri vya migodini, akitaja eneo la mgodi wa uliofungwa wa Buzwagi kama kitovu kinachoweza kuendelezwa kuwa ukanda maalum wa uchumi kwa shughuli hizo.

Pia, amekazia kuwa orodha ya bidhaa na huduma 20 zilizotengwa kwa Watanzania pekee katika migodi itaendelea kulindwa bila mabadiliko, akibainisha kuwa Serikali inalenga kulinda maslahi ya wazawa kwa kuzingatia sheria zilizopo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Steven Kiruswa amesema kuwa pamoja na juhudi za kuvutia wawekezaji, Serikali inaweka mkazo katika madini muhimu na ya kimkakati ambayo yanaendelea kuwa na soko kubwa katika zama za mabadiliko ya teknolojia na mazingira duniani.

Naye, Katibu Mkuu wa TCM, Eng. Benjamin Mchwampaka, ameipongeza Serikali kwa hatua zake za kushughulikia changamoto za sekta hiyo na kudumisha ushirikiano thabiti na sekta binafsi, ameshauri kuwa Serikali inapaswa kudumisha uthabiti wa Sera, Sheria na moiongozo ya Sekta ya Madini, kwani mabadiliko ya mara kwa mara kwani huchelewesha maamuzi ya uwekezaji na kwamba mazingira ya kisheria yanayotabirika yanaongeza ushindani wa nchi, huvutia uwekezaji wa muda mrefu, na kuhakikisha rasilimali za madini zinachangia kikamilifu ukuaji endelevu wa uchumi.

Kwa upande wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Eng. Yahya Samamba amebainisha kuwa mpango maalum unaandaliwa kufadhili wataalamu wa Kitanzania kujifunza katika fani za kisasa kama uchumi wa madini (Mineral Economy), ili kuendana na mahitaji pamoja na  mabadiliko ya kimataifa na kuongeza ushindani wa nchi.

Kwa ujumla, kikao hicho kimeonesha dhamira ya dhati ya Serikali na wadau wa Sekta ya Madini kujenga msingi imara utakaowezesha sekta hiyo kuwa moja ya injini ya uchumi wa Tanzania kuelekea 2050.
Posted by MROKI On Tuesday, April 21, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo