Nafasi Ya Matangazo

April 14, 2026

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wafanyakazi wa sekta ya umma na sekta binafsi katika kukuza uchumi na maendeleo ya Taifa.
 
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu ameyasema hayo jana jioni Aprili 13, 2026 jijini Dodoma katika Hafla ya Maandalizi ya Mei Mosi, 2026 ambayo Kitaifa inafanyika mkoani Njombe.
 
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea kuwaenzi wafanyakazi nchini kutokana na umuhimu wao mkubwa kwa Taifa.
 
Katika hafla hiyo ya awali, kiashi cha shilingi bilioni 1.105 kimekusanywa ambapo Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu alisema fedha hizo zitausaidia mkoa mwenyeji kukamilisha shughuli za maandalizi kwa ajili ya tukio hilo.
 
Mheshimiwa Waziri Mkuu aliongeza kwa kulipongeza Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) kwa ubunifu wa kuhakikisha maadhimisho ya Mei Mosi yanaacha alama katika mkoa mwenyeji.
 
“Wenzetu TUCTA wamekuja na ubunifu kwamba shughuli za Mei Mosi zinaacha alama katika mkoa husika kwa kutekeleza miradi mbalimbali kama walivyofanya katika maadhimisho ya mwaka 2025 mkoani Singida kwa kujenga uwanja wa Bombadia mkoani humo, uwanja ambao sasa umekuwa na manufaa makubwa kwa Wanasingida, na Njombe nako wamejiandaa kuacha alama kubwa.”  Alisema Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba.
 
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Clement Sangu alisema maandalizi ya maonesho ya Mei Mosi mwaka huu yanaendelea vizuri akisisitiza kuwa kwa siku zilizosalia, maandalizi yote yatakamilika ndani ya wakati.
 
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mheshimiwa Anthony Mtaka alisema maadhimisho hayo ni fursa kubwa si tu kwa kwa mkoa wa Njombe, bali kwa mikoa yote ya kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwani ugeni wa watu wasiopungua elfu tano unatarajiwa kushiriki sherehe za Mei Mosi Kitaifa mkoani humo.
 
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), Tumaini Nyamhokya alishukuru na kupongeza kuimarika ushirikiano kati ya Serikali na Vyama vya Wafanyakazi, akisema ushirikiano huo umechangia kuwepo kwa utulivu miongoni mwa wafanyakazi nchini.
Posted by MROKI On Tuesday, April 14, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo