Nafasi Ya Matangazo

March 04, 2026







Na Eleuteri Mangi, WANMM- Bariadi, Simiyu
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanzisha Kliniki Maalumu ya Wanawake “Samia Ardhi Kliniki” hatua inayoweka mazingira rafiki kwa wanawake wengi kumiliki ardhi kisheria sambamba na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na maendeleo. 

Wanawake wa Mkoa wa Simiyu ambao ni miongoni mwa wanufaika wa kliniki hiyo wameishukuru Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuwapelekea Samia Ardhi Kliniki inayoendelea kuwahudumia wanawake na kutatua changamoto zinazowakabili katika umiliki wa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kliniki hiyo Machi 4, 2026 mjini Bariadi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha amesema, Kliniki hiyo imekuja muda muafaka kwa kuwa itasaidia wanawake wa mkoa huo kumiliki ardhi. 

Pia Mkuu wa Mkoa Mhe. Macha ametoa wito kwa wanawake katika mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika wiki ya Samia Ardhi Kliniki ili kupata elimu, ushauri na huduma mbalimbali za Sekta ya Ardhi ikiwemo kupimiwa maeneo yao na kupata Hati Miliki zao. 

Pamoja na uwepo wa Sera na Sheria zinazolinda haki za wanawake, takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 28 pekee ya wanawake nchini ndio wenye hati miliki katika maeneo mbalimbali nchini.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi wakati wa ufunguzi wa Kliniki hiyo, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Simiyu Bw. Denis Masami amesema, hadi kufikia tarehe 4 Machi 2026 wametoa jumla ya Hati 198 na kuweka bayana kuwa, kliniki hiyo inayotarajiwa kuhitimishwa Machi 7, 2026 ni sehemu ya kuelekea maadhimisho Siku ya Kimataifa ya Wanawake ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 08.

Ameongeza kuwa, Mkoa wa Simiyu una lengo la kutoa hati 3,000 kwa mwaka 2025/2026 ambapo hadi sasa wametoa jumla ya hati 1,441 sawa na asilimia 48 ya lengo ambapo kati ya hati hizo 403 ni za wanawake sawa na asilimia 28 ya hati zote zilizotolewa katika mkoa huo.

Kwa upande wake Bi. Stela Manyonyi kutoka Wilaya ya Busega mkoani Simiyu ameahidi kuitumia hati aliyoipata katika shughuli za maendeleo kwa kuchukulia mkopo wa kuendeleza biashara zake.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake mwaka huu ya  inahimiza "Haki sawa kwa Wanawake na Wasichana; Msingi Jumuishi kifikia Dira 2050" huku Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikisisitiza kuwa “Mwanamke; Haki Yako, Miliki Ardhi Sasa’’.
Posted by MROKI On Wednesday, March 04, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo