Nafasi Ya Matangazo

January 27, 2026

image.png
Mwenyekiti wa Waganga Wakuu wa Mikoa, Dkt.Besti Magoma akizungumza wakati wa mafunzo hayo.

image.png
Dkt.Besti Magoma,Mwenyekiti wa Waganga Wakuu wa Mikoa.

Na Mwandishi wetu
Mwenyekiti wa Waganga Wakuu wa Mikoa nchini, Dkt. Best Magoma, amesema mafunzo kwa Viongozi Wasimamizi wa Huduma za Chanjo ngazi ya Mikoa na Halmashauri (Mid-Level Managers, MLM training) ni nguzo muhimu katika kuimarisha ufanisi wa utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Chanjo kuanzia ngazi ya Mikoa hadi vituo vya kutolea huduma za afya.

Dkt. Magoma ameyasema hayo  leo tarehe 26, Januari, 2026  wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalum kwa Viongozi Wasimamizi wa Huduma za Chanjo  yanayofanyika mkoani Iringa kuanzia tarehe 26 hadi 30 Januari, 2026 kwa kuhusisha Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wakuu wa Halmashauri na Makatibu wa Afya wa Mikoa na Halmashauri kutoka Mikoa ya Iringa, Dodoma, Njombe na Morogoro.

Dkt. Magoma amesema anaona tija ya mafunzo haya katika kuongeza uwezo Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri pamoja na wasimamizi wengine wa afya katika kupanga, kusimamia na kutathmini huduma za chanjo kwa ufanisi, kwa kuzingatia matumizi sahihi ya takwimu, usimamizi wa rasilimali na ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli za chanjo.

“Viongozi Wasimamizi wa huduma za chanjo katika ngazi ya kati  yaani Mikoa na Halmashauri ni kiungo muhimu kati ya Sera za kitaifa na utekelezaji wa huduma za afya kwa wanufaika wanaopata huduma hizi katika vituo vya kutolea huduma za afya na ngazi ya jamii.

 Mafunzo haya yanawawezesha kufanya maamuzi sahihi yanayotokana na ushahidi na hivyo kuongeza ufanisi na ubora wa huduma za chanjo,” amesema Dkt. Magoma.

Ameongeza kuwa changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa huduma za chanjo ikiwemo upotevu wa chanjo, usimamizi wa mnyororo baridi pamoja na ufuatiliaji wa watoto waliokosa chanjo, zinaweza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa kupitia mafunzo endelevu kwa wasimamizi wa huduma.
image.png
Kwa upande wake, Afisa Programu kutoka Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dkt. Tumaini Haonga, amesema mafunzo ya MLM ni sehemu ya mkakati wa Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI unaolenga kuimarisha uongozi na usimamizi wa huduma za Chanjo ili kuhakikisha huduma zinafika kwa wananchi wote kwa kuzingatia vigezo vya ubora na usalama wa chanjo.

Dkt. Haonga ameeleza kuwa mafunzo hayo yanajikita katika maeneo muhimu ikiwemo upangaji wa mipango ya utoaji wa huduma za chanjo, matumizi ya taarifa na takwimu za chanjo katika kufanya maamuzi, elimu kwa umma na ushirikishaji wa jamii, usimamizi wa rasilimali watu pamoja na ufuatiliaji na tathmini ya viashiria vya utendaji wa huduma za chanjo.

“Viongozi Wasimamizi wa huduma za chanjo ngazi ya Mkoa na Halmashauri ndio uti wa mgongo wa utekelezaji wa Mpango wa  Taifa ya Chanjo.

Kupitia mafunzo haya tunatarajia kuona ongezeko la viwango vya kuwafikia walengwa na kuwapa huduma ya chanjo kadri ya Miongozo, kupungua kwa idadi ya watoto wanaokosa chanjo na kuimarika kwa ulinzi wa jamii dhidi ya Magonjwa Yanayozuilika kwa Chanjo,” amesema Dkt. Haonga.

Ameongeza kuwa Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa mafunzo ya aina hiyo ili kujenga mfumo imara wa usimamizi wa huduma za chanjo nchini.
image.png

image.png
Dkt.Tumaini Haonga kutoka Wizara ya Afya,Mpangp wa Taifa wa Chanjo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa elimu na ujuzi walioupata utawasaidia kuboresha mipango ya chanjo katika maeneo yao, kuimarisha usimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa chanjo.

Programu ya Mafunzo ya Viongozi Wasimamizi wa huduma za chanjo ni miongoni mwa jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI katika kuimarisha mfumo wa huduma za chanjo na kuhakikisha watoto wote nchini wanapata chanjo kwa wakati, kwa usalama na kwa usawa.
image.png

image.png
image.png

image.png

Posted by MROKI On Tuesday, January 27, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo