Nafasi Ya Matangazo

September 30, 2025

Mtendaji Mkuu Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) Dkt. Naiz Majani na Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire wakibadilishana hati ya mkataba wa ushirikiano wa kusaidia matibabu ya moyo kwa watoto wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo katika ukumbi wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam. 
Mtendaji Mkuu Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) Dkt. Naiz Majani na Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire wakionesha hati ya mkataba wa ushirikiano wa kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo katika ukumbi wa JKCI iliyopo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa JKCI Dkt. Peter Kisenge

Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania zimesaini hati ya makubaliano maalumu ya kusaidia matibabu ya moyo kwa watoto nchini hususan wale wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu hayo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Makubaliano hayo yaliyosainiwa leo jijini Dar es Salaam yanahusisha kusaidia matibabu kwa watoto wenye matatizo ya moyo na kukarabati wodi ya watoto wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).

Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge aliipongeza Vodacom kushiriki katika kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo na kuunga jitihada zinazofanywa na Serikali kuhakikisha matibabu ya moyo yanapatikana nchini.

“Ushirikiano huu utasaidia sana kuwafikia watoto wenye magonjwa ya moyo wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu lakini pia utasaidia kukarabati wodi ya watoto wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) hivyo kuongeza nafasi ya kutoa huduma,” alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge alisema takwimu zinaonesha kuwa kati ya watoto 10,000 huzaliwa nchini wakiwa na matatizo ya moyo kila mwaka, ambapo zaidi ya 4,000 huhitaji upasuaji wa haraka.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Heart Team Africa Foundation (HTAF) Dkt. Naizi Majani alisema mkataba wa HTAF na Vodacom umelenga kuhakikisha kuwa watoto wanaotoka katika familia duni wanapata huduma za matibabu JKCI.

“Lengo letu ni kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo ambao wengi wao hukosa msaada ukilinganisha na watu wazima ambao hupata msaada kutoka kwa watu wengi wanaowazunguka, hivyo makubaliano yetu ni kuhakikisha tunarudisha furaha kwa watoto ambao wanapitia maumivu makali yanayotokana na maradhi ya moyo”, alisema Dkt. Naiz.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire alisema Vodacom imefanya tathmini na kuona kuwa gharama za matibabu hazipaswi kuwa kikwazo cha kuokoa maisha ya watoto hivyo ikaamua kushirikian na HTAF kuokoa maisha ya watoto wanaohitaji upasuaji wa moyo.

“Tupo hapa leo kuiunga mkoni Serikali ya Tanzania kwa kusaidia watoto 150 wenye magonjwa ya moyo kupata matibabu na kurejesha matumaini kwa familia zao kwani kila mtoto anastahili nafasi ya kuishi bila kujali uwezo wa familia zao”, alisema Besiimire.

Kupitia makubaliano hayo HTAF na Vodacom wanatarajia kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto nchini, hatua itakayosaidia kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo kwa watoto.

Mtendaji Mkuu Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) Dkt. Naiz Majani akimuelezea huduma zinazotolewa katika kliniki ya watoto wenye magonjwa ya moyo Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo wakati wa kusaini hati ya mkataba wa ushirikiano wa kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela akimuonesha mmoja wa watoto waliopatiwa huduma katika Taasisi hiyo Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire alipotembelea JKCI leo wakati wa kusaini hati ya mkataba wa ushirikiano wa kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire wakimsikiliza Daktari bingwa wa wagonjwa wa dharura na mahututi wa JKCI Vivian Mlawi walipotembelea wodi ya watoto wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kabla ya kusaini hati ya mkataba wa ushirikiano na Taasisi isiyo ya Serikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire na Mtendaji Mkuu Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) Dkt. Naiz Majani kabla ya kusaini hati ya mkataba wa ushirikiano na HTAF kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo leo jijini Dar es Salaam. Picha na JKCI

 

Posted by MROKI On Tuesday, September 30, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo