
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wakulima wa zao la pamba kufuata miongozo inayotolewa na Serikali kuhusu maendeleo ya zao hilo, akisisitiza kuwa lina maslahi mapana kwa ustawi wa wakulima na uchumi wa nchi.
Akizungumza leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja cha stendi ya mabasi ya wilayani Itilima, Rais Dkt. Samia amesema pamba ni zao lililokuwa limegubikwa na siasa nyingi, hivyo kufuata miongozo ya Serikali kutawawezesha wananchi na Taifa kunufaika na zao hilo.
Rais Dkt. Samia pia amesema Serikali imetenga Shilingi Bilioni 8 kama ruzuku ya uendeleza kilimo cha pamba, zilizoiwezesha kuchukua hatua madhubuti ya kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora na pembejeo kwa wakati.
Katika kukuza uwekezaji kwenye mnyororo wa thamani wa zao hilo, Rais Dkt. Samia amesema Serikali itaendelea kutenga maeneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata pamba mkoani Simiyu, ikiwa ni mkakati wa kuhimiza wawekezaji wa ndani na nje kuanzisha viwanda vitakavyoongeza thamani ya mazao na kutoa ajira zaidi kwa wananchi.
Akizungumzia maendeleo ya miundombinu ya nishati, Rais Dkt. Samia amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Shinyanga hadi Simiyu pamoja na ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme katika mkoa huo, ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika kwa matumizi ya nyumbani na shughuli za uzalishaji viwandani.
Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, Rais Dkt. Samia amebainisha kuwa Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maji katika Wilaya ya Itilima, ikiwa ni pamoja na miradi ya visima na mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria, utakaonufaisha zaidi ya wananchi 495,000 katika Mkoa wa Simiyu.
Mapema leo, Rais Dkt. Samia aliendelea na ziara yake kwa kuzindua kiwanda cha kuchakata pamba hai cha Biosustain Tanzania Ltd wilayani Meatu, na kufungua Hospitali ya Wilaya ya Itilima ambayo itawapunguzia wananchi gharama ya kupata matibabu kutoka katika hospitali nyingine za mikoa jirani.
Sehemu ya
Wananchi wa Meatu waliohudhuria mkutano wa hadhara wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan uliofanyika katika viwanja
vya Stendi ya mabasi tarehe 17 Juni, 2025.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe
0 comments:
Post a Comment