WIZARA ya Maliasili na Utalii imepongeza hatua kubwa iliyofikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kujiandaa kupokea wageni wa mashindano ya AFCON 2027, baada ya Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Bw. Daniel Pancrasi, kujionea maendeleo makubwa yaliyofanyika katika eneo la utalii la Ziwa Duluti, Arusha.
Bw. Pancrasi alitoa pongezi hizo alipofanya ukaguzi wa maandalizi ya miundombinu na huduma zinazotekelezwa na TFS, akisema ameridhishwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa hususan katika maeneo ya malazi, huduma za chakula na kuboresha mazingira ya utalii kwa viwango vinavyoweza kupokea wageni wa kimataifa wakati wa AFCON.
“Hongereni sana TFS. Kwa muda mrefu mmekuwa mkituletea taarifa mbalimbali kuhusu maandalizi haya, lakini leo nimejionea mwenyewe kazi kubwa iliyofanyika. Hakika nimefurahishwa sana. Nitakuwa shahidi katika vikao mbalimbali kwamba TFS haisemi tu kwa maneno, bali inafanya kazi kwa vitendo,” alisema Bw. Pancrasi huku akisisitiza kuwa maandalizi hayo yanaonesha dhamira ya Serikali kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na fursa za kiuchumi zitakazotokana na AFCON 2027.
Alisema maboresho yaliyofanyika Ziwa Duluti yanaongeza hadhi ya vivutio vya utalii vya Tanzania na kuweka mazingira bora ya kuwahudumia wageni kutoka mataifa mbalimbali watakaowasili nchini wakati wa mashindano hayo.
Awali, Mkuu wa Dawati la Utalii wa TFS, Mhifadhi Mkuu, PCO Someni Mteleka, alisema maboresho yanayotekelezwa katika Ziwa Duluti ni sehemu ya mkakati mpana wa TFS wa kuandaa vivutio vya utalii vinavyosimamiwa na wakala huo ili viwe tayari kupokea idadi kubwa ya wageni wakati wa AFCON 2027.
Mteleka alisema uwekezaji unaoendelea unalenga kuboresha ubora wa huduma za malazi, migahawa, mapokezi ya wageni na shughuli mbalimbali za utalii wa asili, sambamba na kuhakikisha wageni wanapata huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Aliongeza kuwa TFS inaendelea kutekeleza maagizo ya Serikali ya kutumia AFCON 2027 kama jukwaa la kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vivutio vya utalii, huku Ziwa Duluti likiwa miongoni mwa maeneo yaliyopangwa kuwa kitovu cha mapumziko na burudani kwa wageni watakaofika nchini.
Ziara ya Bw. Pancrasi imeongeza matumaini kuwa kasi ya maboresho inayoendelea katika vivutio vya utalii vinavyosimamiwa na TFS itaifanya Tanzania kuwa tayari kupokea maelfu ya wageni wa AFCON 2027, huku Ziwa Duluti likitajwa kuwa mfano wa namna uwekezaji wa kimkakati unavyoweza kubadilisha vivutio vya utalii kuwa bidhaa zinazoweza kushindana katika soko la kimataifa.








0 comments:
Post a Comment