Nafasi Ya Matangazo

February 03, 2025

Mjumbe wa Tuhe Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Asina Omari akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili ya watendaji wa Uboreshaji Mkoa wa Pwani. Mafunzo hayo yamefungwa leo Februari 03,2025 ambapo amewataka watendaji hao kutekeleza jukumu la kuhamasisha wananchi wa maeneo yao kushiriki kwenye uboreshaji kwa kushirikiana na wadau wengine wa uchaguzi.
Mjumbe wa Tuhe Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Magadalena Rwebangira akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili ya watendaji wa Uboreshaji Mkoa wa Tanga. Mafunzo hayo yamefungwa leo Februari 03,2025 ambapo amewataka watendaji hao kutekeleza jukumu la kuhamasisha wananchi wa maeneo yao kushiriki kwenye uboreshaji kwa kushirikiana na wadau wengine wa uchaguzi.
Na Mwandishi wetu, Tanga na Pwani
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura  katika Mikoa ya Tanga na Pwani  kuzingatia Katiba ya nchi, sheria za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na kanuni zake katika utekelezaji wa majukumu yao.
 
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Asina Omari wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi na Maafisa TEHAMA Mkoani Pwani leo Februari 03,2025.
 
“Mnapaswa kutekeleza majukumu mliyopewa kwa kuzingatia Katiba ya nchi, sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na kanuni zilizotungwa chini ya vipengele vya sheria hiyo vinavyohusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,”alisema Mhe. Jaji Asina.
 
Aidha, alitoa wito kwa watendaji hao kuhakikisha kuwa wanaendelea kutumia muda  wao wa ziada kusoma na kupitia maelekezo yote waliyopewa ili kuongeza uelewa zaidi kuhusu wajibu na majukumu yao katika zoezi hili la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
 
“Ni matarajio ya Tume kuwa, mara baada ya zoezi hili kukamilika watu watakaokuwa wamepatiwa kadi watakuwa ni wapiga kura halali wa kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani” amesema Mhe. Jaji Asina.
 
Akifunga mafunzo kama hayo Mkoani Tanga nakuhusisha washiriki kutoka katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, Halmashauri za Miji ya Handeni na  Korogwe, Halmashauri za Wilaya ya Kilindi, Lushoto na Muheza, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Magdalena Rwebangira amewataka watendaji hao kutekeleza jukumu la kuhamasisha wananchi wa maeneo yao kushiriki kwenye uboreshaji kwa kushirikiana na wadau wengine wa uchaguzi.
 
“Mnahimizwa kuhamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao,” alisema Mhe. Rwebangira.
 
Alisisitiza kuwa jukumu la uhamasishaji linawahusu moja kwa moja wao watendaji, kwa kushirikiana na wadau wengine katika maeneo yao kupitia nyenzo mlizo nazo.
 
 “Mabango na vipeperushi mtakavyopewa na Tume mvisambaze mapema katika shehia zote zilizopo katika mikoa yote mitatu ya Unguja. Kazi yenu kubwa ni kusimamia na kuendesha shughuli zote za uboreshaji katika shehia zote” amesema Mhe. Magdalena.
 
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa ya Tanga na Pwani umepangwa kufanyika kuanzia tarehe 13 hadi 19 Februari, 2025 ambapo vituo vitafunguliwa Saa 2:00 asubuhi na kufungwa Saa 12:00 jioni.
Meza Kuu ya Mafunzo kwa Mkoa wa Pwani ikiongoza na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji wa Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk (katikati) akifuatilia mafunzo hayo mkoani Pwani.

Washiriki wa Mafunzo kutika Mkoa wa Pwani wakiwa katika ufungaji wa mafunzo.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele akiwa katika ufungaji wa mafunzo hayo mkoani Tanga.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ndg. Kailima R.K akizungumza jambo na washiriki mkoani Tanga. 

Washiriki wa mafunzo hayo kutoka Mkoa wa Tanga wakifuatilia hotuba ya ufungaji.
Washiriki wa mafunzo hayo kutoka Mkoa wa Tanga wakifuatilia hotuba ya ufungaji.
Mwenyekiti wa Mafunzo kutoka Mkoa wa Tanga, Ndg. Mwanaidi Nondo akizungumza jambo kuhusiana na mafunzo hayo waliyopewa.

Washiriki wakifanya mazoezi kwa vitendo kwa kuandikisha wapiga Kura wapya, kuboresha taarifa  na kufuta waliopoteza sifa. 
Posted by MROKI On Monday, February 03, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo