Nafasi Ya Matangazo

February 27, 2025








WAKATI masoko ya madini yakifikia 43, mchango wa masoko hayo umeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 8 mwaka 2018/ 2019 hadi Shilingi Bilioni 183 mwaka wa fedha uliomalizika wa 2023/2024.

Akizungumza katika mafunzo ya  matumizi ya mashine maalum ya kupima madini ya metali kwa njia ya MIONZI /X-RAY,  kwa maafisa masoko wa madini Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Venance Kasiki amesema mbali na masoko hayo pia kuna vituo vya ununuzi wa madini 109.

Amesema, “Kwa kuzingatia asilimia kubwa ya mapato yetu katika masoko yanatokana na madini ya dhahabu, na ili tupate maduhuli lazima tutumie  mashine za XRF kupima asilimia (purity) ya madini yanayouzwa. Majibu yanayotokana na XRF yanatumika  kukokotoa mrabaha  na ada ya ukaguzi,”.

Kwa upande wa Meneja wa Biashara ya Madini Sundi Malomo akizungumza amesema kuwa tangu Serikali kupitia Tume ya Madini  kuanzisha masoko ya madini Mei, 2019 kama mkakati wa kuimarisha biashara ya madini nchini, masoko hayo yamekuwa na mchango mkubwa wa kuongeza mapato  ikiwemo kutoa ajira.

“Ili kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli kama mnavyofahamu Sekta ya Madini inatakiwa ichangie asilimia 10 katika Pato la Taifa kwa mwaka wa Fedha 2024/2025,  Tume ya Madini imepewa lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 1, hivyo tumewapa mafunzo maafisa masoko na kuwakumbusha majukumu ya Idara- sehemu ya biashara,”amesema Sundi na kuongeza,

“ Katika mafunzo haya tumeweza kuainisha changamoto tulizonazo na kuweza kuonyesha mchango wa masoko kuanzia mwaka 2018/2019 ambapo mchango wa masoko ulikuwa ni Shilingi Bilioni 8, mchango huo umeongezeka kwa kiasi kikubwa  mwaka hadi mwaka, mwaka wa fedha 2023/2024 masoko haya yameweza kuchangia takribani Shilingi Bilioni 183,”amesema Sundi.

Katika hatua nyingine,  Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Venance Kasiki amesema ili kuhakikisha mashine za XRF zinatumika vizuri na lengo kusudiwa linapatikana, wameamua kufanya mafunzo kwa watumiaji wa vifaa hivyo waliopo kwenye masoko ya madini mikoa yote ya Tanzania Bara . 

Aidha, amesema wamemualika mtaalam kutoka Kampuni ya Thermo Fisher Scientific ya Afrika Kusini ambao ndio watengenezaji wa mashine hizo,  Mirko Steinhage kutoa elimu zaidi juu ya matumizi sahihi ya XRF.

Kwa upande wake Kaimu Meneja Ukaguzi Madini na Huduma za Maabara, Mhandisi Mvunilwa Mwarabu amesema mafunzo hayo ni fursa njema kwa kuwa mashine za XRF na Mizani ndio vinasaidia katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali hivyo ni muhimu zikatumika kwa ubora ili kubaini kiasi sahihi cha madini na Serikali ipate mapato yake sahihi.

Amesema,  ni imani yake kuwa  baada ya mafunzo hayo vifaa vitatumika kwa usahihi, tija na kasi ya ukusanyaji maduhuli itaongezeka.
Posted by MROKI On Thursday, February 27, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo