MAKUSANYO ya maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini katika Mkoa wa Iringa yatokanayo na mrahaba, tozo na ada mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 yamefikia shilingi milioni 698.05 ikiwa ni asilimia 58.2 ya lengo walilowekewa.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi AbdulRahman Milandu amesema Mkoa wa Iringa umewekewa lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 1.2.
“Mwaka huu wa fedha mpaka sasa tunakaribia asilimia 60, tumekusanya shilingi milioni 698.05 zaidi ya nusu ya lengo, hii inaonyesha fursa zipo,” amesema na kuongeza,
Aidha, Mhandisi Milandu ametoa wito kwa wawekezaji wote nchini kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini mkoani Iringa ambapo mkoa huo umebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali ikiwemo dhahabu, vito, chuma, madini ya viwandani na madini ya ujenzi.
“Madini ujenzi yapo tele wawekezaji waje kuwekeza, pia tuna maeneo ya dhahabu kama Nyakavangala, Ifunda, Kitengulinyi, kijiji cha Sinai na Igoma Wilayani Mufundi yana fursa ya madini ya kutosha ya dhahabu hivyo wawekezaji wakubwa waje kuwekeza,”amesisitiza.
0 comments:
Post a Comment