Nafasi Ya Matangazo

February 19, 2025




Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) taifa ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mlezi wa CCM Mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amewataka Wanachama wa Chama hicho kusimama kifua mbele katika kuyasema mazuri yanayofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 19 Februari, 2025 wakati akizungumza na Wana-CCM mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja iliyokuwa na lengo la kukagua miradi mbalimbali ya Chama hicho katika Mkoa huo.

Aidha, Dkt. Tulia amewasisitiza Wanachama wa Chama hicho kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura katika tarehe zilizopangwa ili kufanikisha ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025.

Dkt. Tulia amesisitiza umuhimu wa Wanachama hao kuendelea kuwa wamoja wakati wote na kuepuka kutengeneza makundi yasiyo na tija kwa Chama na taifa. Kufanya hayo itasaidia kuunga mkono kazi nzuri inayofanywa na Chama hicho chini ya Viongozi wao wakuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapunduzi Zanzibar.

Sambamba na hayo, Dkt. Tulia ametoa mchango wa Shilingi Milioni tano (Tsh: 5,000,000/-) kwa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Kaskazini Unguja ili kuunga mkono ujenzi wa jengo la kitega Uchumi la Wanachama hao.


Posted by MROKI On Wednesday, February 19, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo