Maisha ya Watanzania wengi yamebadilika kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ( HESLB) katika kuwawezesha kufikia ndoto zao za kielimu na kimaisha baada ya kunufaika na mikopo ya elimu ya juu.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia kwenye maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa Bodi ya Mikopo yaliyofanyika Februari 15, 2025 kwenye viwanja vya Farasi, Oysterbay, jijini Dar es Salaam ambapo maadhimisho hayo yaliambatana na mbio za hisani ( HESLB Marathon).
Katika hotuba yake iliyojaa takwimu za kimafanikio kuhusiana na miongo miwili (miaka 20) tangu kuanzishwa Bodi ya Mikopo, Dk. Kiwia amesema wakati Bodi ya Mikopo inaanzishwa mwaka 2004, ni wanafunzi 48,000 pekee ndiyo waliokuwa wakinufaika, ambapo bajeti yake ilikuwa Bilioni 53.1. Aidha Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Bodi imetoa mikopo kwa wanafunzi 245,799 huku mikopo hiyo ikigharimu Bilioni 787, na kwa ujumla wake, katika miaka 20 ya Bodi, jumla ya wanufaika wote imefika 830,000 huku mikopo yote iliyotolewa ikigharimu Trilioni 8.2.
"Kwa mwaka 2024/2025, shilingi Bilioni 787 zimetolewa kwa ajili ya wanafunzi 245,799 ambapo jumla ya mikopo iliyotolewa na Bodi tangu kuanzishwa kwake ni shilingi Trilioni 8.2 ambacho kimewezesha kusomesha wanafunzi 830,000 nchi nzima," amesisitiza Dk. Kiwia.
Mbio hizo za hisani za HESLB Marathon zilifana ambapo watu mbalimbali walijitokeza kushiriki huku wengi wakipongeza kazi nzuri zilizofanywa na Bodi ya Mikopo katika kipindi cha miaka 20 zilizowezesha vijana wengi kupata elimu ya juu.
0 comments:
Post a Comment