Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesema kuwa mapambano ya uhuru wa kiuchumi na ustawi wa kijamii katika nchi za Kusini mwa Afrika yanaendelea kwa kasi kubwa, ikiwa ni njia ya kuwaenzi waasisi wa ukombozi wa kisiasa katika ukanda huo.
Akizungumza katika tukio la utoaji heshima za mwisho kwa Rais wa Kwanza wa Namibia na Baba wa Taifa hilo, Mhe. Dkt. Sam Shafiishuna Nujoma, lililofanyika tarehe 27 Februari 2025 katika Uwanja wa Sam Nujoma, jijini Windhoek, Balozi Nchimbi alisema kuwa kizazi cha sasa cha viongozi wa ukanda huo, pamoja na vyama vilivyoongoza harakati za ukombozi, kinaendelea kuthamini na kuenzi jitihada za waasisi wa uhuru.
Alisisitiza kuwa waasisi hao walijitoa kupigania misingi ya utu wa binadamu, demokrasia, Umoja wa Afrika, uhuru wa kujitawala, amani, na mshikamano—misingi ambayo ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya watu wote barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na maelfu ya waombolezaji, wakiwemo viongozi wakuu wa chama tawala cha Namibia, SWAPO.
Miongoni mwao walikuwa Makamu wa Rais wa SWAPO, Komredi Netumbo Ndemupelila Nandi Ndaitwah, ambaye pia ni Rais Mteule wa Namibia, pamoja na Katibu Mkuu wa SWAPO, Komredi Sophia Shaningwa. Familia ya Hayati Sam Nujoma pia ilihudhuria tukio hilo, sambamba na viongozi wa vyama mbalimbali rafiki.
Balozi Nchimbi alieleza masikitiko yake kwa kifo cha Mhe. Dkt. Nujoma, akisema:
“Taarifa za kifo cha Rais Nujoma zilitusikitisha sana. Tulipopata habari hizi tulishtuka sana. Alikuwa kiongozi pekee aliyebaki hai miongoni mwa waasisi wa ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, na mmoja wa waasisi wa Nchi za Mstari wa Mbele. Alikuwa amana yetu iliyobaki ya hekima na alama ya ukombozi wetu. Tunahisi kuibiwa. Tunahisi kupotea!”
Akitafakari mchango wa Hayati Dkt. Nujoma katika harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika, Balozi Nchimbi alieleza kuwa ushindi wa Namibia dhidi ya ukoloni ulikuwa wa kimkakati kwa mataifa ya mstari wa mbele. Kupata uhuru kwa Namibia kulitoa fursa muhimu ya kuendeleza mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi wa makaburu nchini Afrika Kusini.
“Rais Nujoma ni miongoni mwa viongozi waasisi wa Afrika waliokomboa nchi zao na wakaachia madaraka kwa hiyari na kidemokrasia. Kwa kufanya hivyo, aliiweka Namibia kwenye njia sahihi ya demokrasia na uongozi wa amani. Hilo linaeleza kwa nini Namibia leo hii ni mfano bora wa demokrasia barani Afrika. Huu ni urithi wake wa kudumu,” aliongeza Balozi Nchimbi.
Akirejea kumbukumbu za harakati za ukombozi wa Afrika, Balozi Nchimbi alifichua jinsi Mzee Nujoma alivyolazimika kwenda uhamishoni wakati wa mapambano ya uhuru wa Namibia, akitumia pasipoti ya Tanzania yenye jina la Samuel Mwakangale. Hii ni ishara ya namna Tanzania ilivyokuwa ngome salama kwa SWAPO na harakati za ukombozi kwa ujumla.
Balozi Nchimbi pia alinukuu salaam za Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa watu wa Namibia, akimwelezea Dkt. Nujoma kama:
“Mpigania uhuru, Mwafrika shupavu, na rafiki wa kweli wa Tanzania, ambaye aliwahi kuishi hapa wakati wa harakati za ukombozi wa Namibia. Aliishi maisha ya utumishi, yaliyounda mstakabali na mwelekeo wa nchi yake, huku akihamasisha vizazi kusimama kwa ajili ya maadili ya uhuru, usawa, na haki.”
Katika hitimisho lake, Balozi Nchimbi aliwasilisha ujumbe wa heshima kwa waasisi wa ukombozi wa Afrika waliotangulia mbele za haki:
“Nembo yetu ya mwisho imeondoka. Shujaa wetu wa mwisho ameanguka. Kiongozi wetu wa mwisho wa nchi za mstari wa mbele ameenda kuungana na wenzake. Komredi Nujoma, tafadhali tunakuomba utufikishie salaam za heshima kwa Julius Nyerere, Agostinho Neto, Samora Machel, Kenneth Kaunda, Robert Mugabe, na Nelson Mandela. Tunawashukuru kwa kutuletea uhuru wa kisiasa. Waambie kuwa mapambano ya ustawi wa kiuchumi Kusini mwa Afrika yanaendelea!”
Mazishi ya kitaifa ya Hayati Dkt. Sam Nujoma yamepangwa kufanyika tarehe 1 Machi 2025, katika eneo la makaburi ya mashujaa, jijini Windhoek, baada ya kuagwa rasmi kitaifa tarehe 28 Februari 2025, ambapo yakihudhuriwa na viongozi wa ndani na nje ya Namibia.
0 comments:
Post a Comment