Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Wathamini nchini kupunguza migogoro inayotokana na uthamini kwa kuhakikisha thamani halisi ya ardhi inayofanyiwa uthamini inajulikana.
Mhe. Ndejembi amesema hayo baada ya kutunuku vyeti vya Taaluma ya Uthamini Wathamini waliohitimu mafunzo ya taaluma hiyo kwenye mahafali ya nne yaliyoenda sanjari na mkutano wa tano wa mwaka wa Bodi ya Usajili wa Wathamini (VRB) Desemba 4, 2024 jijini Dodoma.
Amesema, teknolojia inabadilika katika nyanja mbalimbali ikiwemo njia ya mawasiliano, namna ya kufanya kazi na biashara ambapo ameweka wazi kuwa, taaluma ya uthamini nayo haiko nyuma na inapaswa kuendana na mabadiliko hayo.
“Kama wathamini, ni muhimu mjikite katika matumizi ya zana za kidijitali zinazopatikana kwenu, kutoka kwa mifumo ya Kijiografia (GIS), Akili Bandia (AI), na Mifumo mbalimbali ya kidijitali. Teknolojia hizi zinawapa uwezo wa kufanya uthamini za ardhi na mali kwa usahihi zaidi na kwa ufanisi zaidi” amesema Waziri Ndejembi.
Waziri Ndejembi amewataka wathamini kuunganisha teknolojia katika kazi zao za kila siku kwa kuwa kunaboresha usahihi wa kazi za uthamini sambamba na kuimarisha uaminifu wa taaluma hiyo ili kukuza uwazi na haki, jambo ambalo alilolieleza linajenga imani miongoni mwa wawekezaji, taasisi za serikali, na jamii kwa ujumla.
“Hivyo, nawaasa kila mmoja wenu kujitahidi kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia, kuwekeza katika maendeleo yenu ya kitaaluma na majukwaa mbalimbali ya kidijitali ambayo yanaweza kuboresha kazi zenu” amesema Waziri Ndejembi.
Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Wathamini nchini Bw. Joseph Shewiyo amesema, kwa sasa kuna zaidi ya Wathamini 400 nchini ambapo kupitia mahafali hayo jumla ya wahitimu 34 wamehitimu.
Mkutano huo wa mwaka wa Bodi ya Usajili wa Uthamini (VRB) unaongozwa na Kaulimbiu “Mwelekeo wa Uthamini Tanzania; Kujumuisha Teknolojia, Uvumbuzi na Ustahimilivu wa Mazingira” kaulimbiu inayohimiza kuendelea kuzingatia mabadiliko ya kimataifa na maendeleo ya kiteknolojia kwa kuzingatia umuhimu wa uendelevu na ustahimilivu wa mazingira katika utendaji kazi wa wataaluma hao.
0 comments:
Post a Comment