Nafasi Ya Matangazo

October 05, 2024


Ataka fedha za ndani zitumike katika kutekeleza miradi ndani ya halmashauri.

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka maafisa masuhuli kwenye Halmashauri zote nchini waweke msisitizo wa kutumia mifumo ya kielektroniki katika makusanyo badala la kukusanya kwa fedha taslimu ‘Cash’.

Amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza mapato katika maeneo yao na kuepuka vishawishi vya kutumia vibaya fedha za umma ambazo zinakusanywa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Amesema hayo leo (Jumamosi, Oktoba 05, 2024) alipozungumza kwenye kikao na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam. “Suala la mapato ni lazima mliwekee msisitizo ili tupate matokeo mazuri kwenye halmashauri zetu. ”

Mheshimiwa Majaliwa pia ametoa wito kwa wakurugenzi wa Halmashauri kutumia mapato ya ndani katika kutekeleza miradi ya maendeleo badala ya kusubiri fedha kutoka Serikali kuu pekee.

“Acheni kutegemea mapato ya Serikali kuu pekee, tunataka kuona mapato ya ndani yanatumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo. ”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uaminifu ili mipango na malengo ya Serikali ya kuwahudumia Watanzania yaweze kutimia. 

Amesema kuwa  watumishi wa umma ni wahudumu wa wananchi hivyo wanapaswa kuwahudumia ipasavyo kwenye maeneo yao na kutatua kero zao. “Sisi tunataka tuone mkifanya kazi kwa bidii, uadilifu, uaminifu usipofanya hivyo utakuwa unakosa sifa za kuwa mtumishi wa umma” Amesema Waziri Mkuu.

“Sisi ni watumishi wa umma na ni wahudumu wa Wananchi, tumefunga mikataba ili tuwe wahudumu wao, tumekubaki hilo, twende tukafanye kazi, tunapaswa kuwatembelea walipo, kila mmoja ana wajibu wa kuwahudumia wananchi kwenye maeneo yao. ”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa umma wafanye tathmini ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika maeneo yao kwa kuangalia hatua iliyofikiwa na sehemu iliyobaki ili mpaka kufikia June 2025 miradi hiyo iwe imefikia zaidi ya asilimia 95 ya utekelezaji.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa umma kusimamia maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na kutengeneza mazingira wezeshi ya kujiendeleza kiuchumi.  “Punguzeni urasimu ili tujenge imani kwa  tunao wahudumia, makundi yote yaliyo kwenye maeneo yenu yakiwemo ya vijana, wazee, wanawake na wenye ulemavu lazima tuwafikie na kusimamia uchumi wao”.





Posted by MROKI On Saturday, October 05, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo