Nafasi Ya Matangazo

October 12, 2024






Na Mwandishi Wetu
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imepokea ugeni kutoka nchini Sierra Leone kwa lengo la kujifunza mbinu bora za ujenzi wa barabara za mwendokasi (BRT) pamoja na daraja la Tanzanite. Ugeni huo ulitoka katika taasisi mbalimbali za Wizara ya Ujenzi ya Sierra Leone.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Ephatar Mlavi, amesema wageni hao walitembelea ujenzi wa mradi wa BRT awamu ya 3 unaoanzia Gongolamboto hadi Posta. Wageni hao wamevutiwa na mradi huo kutokana na kwamba nchini kwao hawana mradi kama huo unaopunguza msongamano wa magari.

"Wageni wetu wamekuja kujifunza kutoka kwetu kwa kuwa wanataka kuboresha miundombinu ya barabara kwao. Wameona tunafanya vizuri katika ujenzi wa barabara za mwendokasi na madaraja, kama vile Daraja la Tanzanite na barabara za mzunguko zinazojengwa Dodoma, pamoja na upanuzi wa barabara kwenye miji ya Mbeya, Arusha, na Dar es Salaam," alisema Mha. Mlavi.

Aidha, wageni hao walitembelea Daraja la Tanzanite lililopo Salender, ambapo walijifunza kuhusu ujenzi wa madaraja yanayopita juu ya maji. Pia walijifunza jinsi TANROADS inavyotumia wahandisi wa ndani katika ujenzi wa miundombinu inayounganisha mikoa na maeneo muhimu kwa usafirishaji.

Mhandisi Mlavi aliongeza kuwa mafanikio ya TANROADS yanatokana na wataalam wenye weledi na ushirikiano mzuri kati ya watumishi wa Wakala huo, Serikali Kuu, na Wizara husika, huku akisisitiza umuhimu wa mipango madhubuti katika ujenzi wa miundombinu.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara wa Sierra Leone, Mohamed Kallon, alisema wamejifunza mengi kutoka TANROADS, licha ya kuwa Wakala ya Tanzania ni mchanga zaidi tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, ikilinganishwa na yao iliyoanzishwa mwaka 1992, lakini bado hawajafanikiwa kujenga barabara za kiwango cha Tanzania.

Naye Muelimishaji Umma wa Serikali za Mitaa wa Sierra Leone, Bi. Martha Gbouma, alisema TANROADS imefanya kazi nzuri katika ujenzi wa barabara, na wamepanga kutumia elimu waliyopata kuboresha miundombinu ya barabara nchini kwao.

Mtaalam wa Usimamizi wa Mali za Barabara, Mha. Kingstone Gongera, alisema kuwa ameona jinsi matengenezo ya barabara yanavyofanyika kwa msaada wa Mfuko wa Barabara, jambo ambalo litawasaidia kuboresha utendaji wao nchini Sierra Leone.
Posted by MROKI On Saturday, October 12, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo