Nafasi Ya Matangazo

October 06, 2024

Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow akiongea katika mkutano na waandishi wa habari ,viongozi wa serikali na wadau mbalimbali uliofanyika katika mgodi wa bulyanhulu jana,(Kushoto) ni Naibu Waziri wa Madini, Dk.Steven Kiruswa na (kulia) ni Meneja wa Barrick nchini,Melkiory Ngido.
Naibu Waziri wa Madini, Dk.Steven Kiruswa akiongea katika mkutano huo.
Mbunge wa Nyang'hwale,Mh.Hussein Nasor Amar akiongea katika mkutano huo.

Na Mwandishi Wetu.

Naibu Waziri wa Madini, Dk.Steven Kiruswa, amesema ubia kati ya Kampuni ya Dhahabu ya Barrick na Serikali ya Tanzania ni kielelezo cha mafanikio ya ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi kwa kuwa unazidi kuleta manufaa nchini na ameomgeza kuwa Serikali itaendelea kuwalinda wawekezaji wenye kuleta mapinduzi chanya katika kukuza uchumi wa nchi .

Akiongea na katika mkutano wa waandishi wa habari wa kupokea taarifa ya utendaji wa migodi ya Barrick na Twiga uliojumuisha wadau mbalimbali uliofanyika katika mgodi wa Bulyanhulu, Dk.Kiruswa, alisema ubia huu umekuwa mfano wa kuigwa kwa kuwa migodi yote inayoendeshwa na Barrick uendeshaji wake umekuwa wa uwazi pia mafanikio yake yanaonekana kutokana na kutoa mchango mkubwa kwa Serikali kupitia kodi mbalimbali, kufanikisha miradi ya kijamii kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR), kupanua wigo kwa ajira kwa Watanzania na kunufaisha wananchi kupitia utekelezwaji wa sera ya maudhui ya ndani (Local content kwa ufanisi mkubwa) sambamba na uwekezaji katika matumizi ya teknolojia za kisasa cha uchimbaji.

Alisema Serikali haitafumbia macho vitendo vya kuwahujumu wawekezaji wanaofanya vizuri katika uwekezaji wao nchini kwa lengo la kuwakatisha tamaa na kurudisha nyuma mkakati wa Serikali wa kukuza uwekezaji nchini yakiwemo mashirikika yasio ya Kiserikali ya nje ya nchi ambayo yamekuwa yakijifanya kiranja wa kutetea haki za binadamu na kusambaza taarifa za uwongo dhidi ya wawekezaji wa hapa nchini zikijifanya kuwatetea watanzania wanyonge wakati zinatafuta mianya ya kujinufaisha kupitia mgongo wa watanzania.

“Serikali ya Tanzania iko imara na madhubuti katika kusimamia wawekezaji kuhakikisha wanafuata kanuni na sheria zake kupitia taasisi zake mbalimbali zilizoanzishwa kisheria ambazo zinafanya vizuri na wanaokiuka sheria wanachukuliwa sheria na kupewa maelekeza na miongozo hivyo hayo mashiriki yasio ya Kiserikali yaache kuchafua taswira ya nchi kama ambavyo yamekuwa yakifanya kwa muda mrefu kupitia mgodi wa North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara” ,alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na maombi yaliyokuwa yakitolewa kwa Serikali na viongozi wa wananchi katika maeneo ya migodi ya kuwatengea wachimbaji wadogo maeneo na kuyataka makampuni makubwa yenye teknolojia ya uchimbaji kuwasaidia Serikali imeanza kuyafanyia kazi na imeanza mazungumzo na makampuni makubwa kupitia Wizara ya Madini na taasisi zake zinazosimamia uchimbaji wa madini.

Ubia huo unachangia 51% ya mapato ya Serikali yanayotokana na tasnia ya uchimbaji madini, kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Mpango wa Uwazi wa Tasnia ya Uchimbaji Madini Tanzania (TEITI). Ubia wa Twiga unajumuisha migodi ya dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu.

Migodi yote miwili pia iliongoza katika utendaji wa kiusalama wa tasnia hiyo, huku Bulyanhulu ikishinda Tuzo ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka huu wakati North Mara ikitajwa na Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Tanzania (OSHA) kuwa kampuni bora katika kuwahudumia wafanyakazi wenye mahitaji maalumu.

Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, alisema katika mkutano huo kuwa utafutaji wa madini unaoendelea katika maeneo yaliyotumika na kuachwa karibu na migodi yake ya Bulyanhulu na North Mara unaendelea. Utafiti huo umebainisha fursa zaidi za kuzihuisha na kuzipanua hifadhi za madini ambapo madini yatakwisha au kupungua, jambo litakalosaidia zaidi katika kuongeza uhai na unyumbufu wa migodi hiyo. Aidha, maendeleo mazuri yameshapatikana katika kuyabainisha maeneo mapya ambapo hapakuwahi kuwa na shughuli za uchimbaji madini, yenye uwezo wa kuongeza migodi mipya kwenye kampuni hiyo.

Aidha, Bristow alisema mpango wa Barrick na Twiga wa Kusongesha Mbele Mustakabali wa Elimu umekamilisha awamu yake ya kwanza, ambapo Barrick ilifadhili upanuzi wa miundombinu ya shule zipatazo 64, yenye thamani ya dola milioni 10, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa vipatavyo 396, mabweni yapatayo 97 na majengo ya maliwato yapatayo 600. Awamu ya pili ya mpango huo umepangwa kuanza katika robo ya nne ya mwaka huu kwa uwekezaji mwingine wa dola milioni 10 ambao utafuatiwa na awamu ya tatu ya dola milioni 10.

Wakati huohuo, Chuo cha Barrick, kilichozinduliwa mwanzoni mwa mwaka na Waziri wa Madini kwenye mgodi uliofungwa wa Buzwagi na ambao hivi sasa ni eneo maalum la uzalishaji (SEZ), tayari kimetoa mafunzo kwa mafomeni, wasimamizi na warakibu zaidi ya 1,000 kutoka katika nchi za Afrika na Mashariki ya Kati. Chuo hiki kiko mbioni kufikia lengo lake la kutoa mafunzo kwa zaidi ya watu 2,000 mwaka huu.

Bristow alisema kulingana na dhamira ya uwazi ya Barrick, kampuni hiyo iliwasilisha taarifa za hivi karibuni za mfululizo wa tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu zilizokuwa zinatolewa dhidi ya Mgodi wa North Mara kwenye Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (CHRGG). Baada ya kutembelea mgodi huo na maeneo ya jirani na kufanya uchunguzi wa kina, tume hiyo ilitoa taarifa iliyothibitisha kwamba hapakuwa na ushahidi wa ukiukwaji wa haki za binadamu katika mgodi wa North Mara na hivyo kuuondolea mgodi huo tuhuma hizo zilizotolewa na baadhi ya mashirika yasiyo yasiyo ya kiserikali ya nchi za nje.

Viongozi mbalimbali wa Serikali kutoka wilaya za Kahama, Msalala na Nyang’hwale waliohudhuria mkutano huo, walipongeza mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana kupitia uwekezaji wa Barrick hususani katika kufanikisha miradi mikubwa ya kijamii kupia fedha za uwajibikaji kwa jamii kwenye sekta ya afya na elimu.
Posted by MROKI On Sunday, October 06, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo