Nafasi Ya Matangazo

October 06, 2024













Na Uzeni Madini Bo
*Maonesho ya Madini Geita kuwakutanisha Wawekezaji na wadau Sekta ya Madini*
Tanzania inashika nafasi ya nne kwa uzalishaji wa Madini ya Dhahabu Afrika lakini bahati mbaya haina akiba ya kutosha ya madini hayo ambapo azma ya Serikali ni kuwa na hifadhi ya kutosha ya dhahabu katika Benki  Kuu ya Tanzania.
Hayo ameyasema Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko Oktoba 05, 2024 wakati akifungua Maonesho ya Saba ya Kitaifa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili Mkoani Geita.
 “Tuna madini  Afrika nzima, nchi yetu ni ya nne lakini hatuna akiba ya dhahabu  ya kutosha na nyingi tunapeleka mataifa mengine,”amesema Dkt Biteko na kuongeza,
“Mfumo uliowekwa na Wizara ya Madini, mna mazingira mazuri ya kufanya biashara kuliko wakati wowote ule kwenye historia, ungeni mkono juhudi za Serikali, akiba ya dhahabu itatusaidia kuimarisha shilingi yetu wakati wa msukosuko unapotokea.
“Matatizo mbalimbali yanayotokea, Marekani wameamua kubadilisha Sera yao na wameitisha Dola zote kwenda kwao, sisi na nchi nyingine za Kiafrika tunahaha kupata Dola, utajiri tulionao ni dhahabu lakini hatuna akiba ya kutosha,”amesema Dkt. Biteko.
Aidha, ameipongeza sekta ya madini kwa kuimarisha  ukusanyaji wa mapato na  udhibiti wa mianya ya utoroshaji wa madini na kuwafanya wachimbaji wafanikiwe.
Pia, Dkt. Biteko ametoa wito kwa wananchi kutembelea mabanda mbalimbali katika maonesho hayo ili kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo namna bora ya uchimbaji salama, utafiti, uchenjuaji, uongezaji thamani madini na biashara ya madini.
Amesema lengo la maonesho hayo, ni kuwakutanisha wawekezaji, wachimbaji, wafanyabiashara na wachenjuaji wa madini ili kujifunza shughuli za utafiti na mnyororo mzima wa uongezaji thamani madini.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amempongeza Dkt. Biteko kwa kutenga muda wake na kuja kuungana katika ufunguzi wa maonesho hayo na pia amempongeza Rais wa Tanzania kwa kuiongezea bajeti Wizara ya Madini kwa lengo la kuimarisha sekta hiyo ili iweze kuwahudumia wachimbaji, wachenjuaji na wafanyabiashara wa madini ili wachimbe kwa tija na kunufaika wao pamoja na Taifa kwa ujumla.

Mavunde amesema, Mheshimiwa Rais ameongeza bajeti ya Wizara ya Madini kutoka shilingi bilioni  89 hadi shilingi bilioni 231 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 110.4 zimeelekezwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kusaidia katika utafiti wa kina kwa lengo la kumsaidia mchimbaji kujua maeneo yenye madini, kiasi kilichopo na mwelekeo wa miamba ya madini kwa lengo la kuepusha upotevu wa mitaji.

Pamoja na mambo mengine, Mavunde amesema kuwa majuzi kuna tatizo lilitokea la wafanyabiashara wa madini  kugoma  ambapo hawakuwa tayari kuridhia mabadiliko ya Sheria, ambapo mpaka sasa kikao kimefanyika na kukubaliana kimsingi, hakuna mfanyabiashara atakaegoma, BOT itauziwa dhahabu kwa bei ya soko la dunia na malipo yatalipwa ndani ya saa 24.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigella amesema, Serikali kupitia Wizara ya Madini na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita imekusudia kuyafanya Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini kuwa Maonesho ya Kimataifa ambapo kwa Mwaka 2024 zaidi ya washiriki 816 wameshiriki ikilinganishwa na washiriki 317 walioshiriki Mwaka 2023.
Posted by MROKI On Sunday, October 06, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo