Nafasi Ya Matangazo

October 06, 2024


Na Mwandishi wetu,Geita
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Doto Mashaka Biteko ameipongeza Wizara ya Madini kwa mkakati wanaoutekeleza ambao unawazesha upatikanaji wa  akiba ya Dhahabu  kupitia Benki kuu ya Tanzania jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya Uchumi wa Tanzania.

Hayo yamesemwa jana Oktoba 05 2024 wakati wa ufunguzi wa maonesho ya saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yenye kauli mbiu ya “Matumizi ya Teknolojia sahihi ya Nishati safi  katika sekta ya Madini kwa maendeleo endelevu” yanayofanyika Mkoani Geita. 

“Sisi utajiri ambao Mungu ametujaalia ni utajiri wa madini ikiwemo Dhahabu, lazima madini haya yawe chachu katika ukuaji wa uchumi wetu.

Naipongeza Wizara ya Madini kwa bidii kubwa mlioifanya sasa ya kuanzisha na kusukuma uwepo wa akiba ya Dhahabu kupitia Benki kuu ya Tanzania”, alisema Mh. Biteko. 

Kwa upande wake Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameeleza kwamba kwa sasa baada ya kukaa pamoja baina ya serikali na wadau wamefikia muafaka na hakuna mgomo tena wa kutoiuzia Dhahabu BOT baada ya ufafanuzi wa baadhi ya hoja na elimu kutolewa ikiwa ni sehemu ya falsafa ya maridhiano inayohubiriwa kwa nguvu na Mh Rais Dkt. Samia S. Hassan.

Mh Mavunde ametoa rai kwa wadau wote kushirikiana na serikali katika mpango huu wa upatikanaji wa akiba ya dhahabu kupitia BOT na kuahidi kutoa ushirikiano katika kushughulikia changamoto mbalimbali zitakazojitokeza.

Akitoa maelezo ya awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kukuza Sekta ya Madini hasa kwa Wachimbaji wadogo na kuahidi kwamba Mkoa wa Geita utaendelea kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya madini ambapo mkoa huo ni mzalishaji mkubwa wa madini ya dhahabu.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Kilumbe Shabani Ng’enda ameeleza kuwa Kamati  inaridhishwa na mwenendo wa Wizara ya madini hususani inavyosimamia sheria na sera ya madini kwa manufaa ya uchumi wa watu na nchi kwa ujumla.

Akitoa salamu zake,Rais wa Shirikisho la Vyama cha Wachimbaji Madini(FEMATA) Ndg. John W. Bina ameipongeza Wizara ya madini kwa usikivu na majadiliano ya mara kwa mara pindi changamoto zinapojitokeza na kuahidi kwamba baada ya kikao cha pamoja wadau wameridhia mpango wa serikali wa ununuzi wa dhahabu kupitia BOT.
Posted by MROKI On Sunday, October 06, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo