Nafasi Ya Matangazo

October 27, 2024







WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wahakikishe wanalinda utamaduni na kujenga misingi ya kuhamasisha vijana na vizazi vijavyo kutambua na kuenzi historia na urithi wa Mtanzania.

Amesema kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kutunza utamaduni, mila na desturi kwa sababu utamaduni ni nguzo ya utambulisho wa jamii husika na ni muhimu kwa kizazi kijacho.

Amesema hayo leo (Jumapili, Oktoba 27, 2024) wakati akifungua Tamasha la Buhaya 2024 ‘Buhaya Festival’ lililofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

“Katika siku za sasa, ambapo teknolojia na utandawazi vinazidi kuimarika, ni rahisi kupoteza mila na desturi zetu, hivyo tunaposhiriki tamasha hili, tunajifunza na kuhamasisha jamii zetu kuhusu umuhimu wa urithi wetu wa kiutamaduni.”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewaasa wazazi, jamii na madhehebu ya dini kuendelea kuhimiza utunzaji wa maadili kwa kuzingatia mila na desturi ili kuepuka mmomonyoko wa maadili kwa vijana na jamii kwa ujumla. 

“Watanzania wote tuendelee kuheshimu na kuenzi tamaduni zilizo nzuri kama njia ya kuimarisha umoja, mshikamano na maendeleo ya kiuchumi,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameagiza Mikoa yote nchini kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi iweke mipango ya kuandaa matamasha ya utamaduni kuanzia ngazi za Wilaya ili kuendeleza na kuhifadhi vivutio, mila na desturi za maeneo husika.

Akizungumzia kuhusu Maendeleo ya Mkoa wa Kagera, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo kwenye sekta za nishati, maji, kilimo, uvuvi, Uchukuzi na ujenzi wa barabara.
Posted by MROKI On Sunday, October 27, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo