Nafasi Ya Matangazo

October 16, 2024







Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amekitaka Chuo cha Misitu Olmotonyi kilichopo Jijini Arusha kufanya Utafiti katika Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro Ili kubaini chanzo cha mimea vamizi na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa lengo la kutatua changamoto hiyo inayolikumba eneo hilo.

Agizo hilo amelitoa leo Oktoba 16, 2024 alipofanya ziara ya kikazi Chuoni hapo na kuzungumza na Watumishi wa Chuo hicho katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Olmotonyi.

. "Kwa kuwa hapa tunatoa huduma ya Ushauri wa kitaaalamu na Utafiti wa Misitu na Uhifadhi naomba nielekeze muwasiliane na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ili mfanye tafiti kuhusu namna ya kudhibiti mimea vamizi" alisema Mhe. Chana.

Aidha, katika hatua nyingine Mhe. Chana amekipongeza Chuo hicho kwa kuweza kubuni andiko la uanzishwaji wa miundombinu ya utalii na kuwasisitiza kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kufanikisha lengo hilo na kuwasisitiza kuendelea kuwajengea watumishi uwezo wa kitaalamu wapate masomo ya juu.

Naye, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Masuala ya Utalii,  Nkoba  Mabula amekipongeza Chuo hicho kwa kuwa na maeneo maaalumu yanayoendeleza Utalii na kuahidi kufanya ziara Chuoni hapo kuona maeneo hayo na kutafuta namna ya kuyaendeleza Ili kuvutia Watalii zaidi.

Kwa Upande wake, Mkuu wa Chuo cha Misitu Olmotonyi,  Dkt Joseph Makero ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kukiboresha Chuo hicho pamoja kuongeza idadi ya Watumishi wanaopangiwa kituo cha kazi chuoni hapo.

Aidha, Dkt. Makero amesisitiza kuwa Chuo hicho kitaendelea kuipeperusha vyema Bendera ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwaandaa vyema Wanafunzi wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuendelea kuhifadhi Maliasili na Kutangaza Utalii.

Kikao hicho kimehudhuriwa na baadhi ya Watumishi pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Masuala ya Utalii,  Nkoba  Mabula Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo,Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Edward Kohi.
Posted by MROKI On Wednesday, October 16, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo