Nafasi Ya Matangazo

September 13, 2024








Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amesema Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha kunakuwa na unafuu katika upatikanaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia ikiwemo mitungi ya gesi  ili kumwezesha kila mwananchi  kutumia nishati iliyo safi na salama.

Katika kutekeleza jitihada hizo, Serikali  imetoa ruzuku kwa mitungi ya gesi zaidi ya 400,000 itakayouzwa kwa nusu gharama ya awali ambayo inasambazwa katika mikoa yote Tanzania Bara huku zoezi hilo likiwa ni endelevu. 

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 13 Septemba 2024 jijini Dodoma wakati wa hafla ya Kusainiwa mikataba ya ushirikiano ya utekelezaji wa Nishati Safi ya Kupikia yenye thamani ya shilingi bilioni 50.98 kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na taasisi sita ambazo ni Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Jeshi la Magereza (TPS) na Wasambazaji wa Gesi ya kupikia, hafla ambayo ilienda sambamba na uzinduzi wa jengo la REA.

“Namshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake yanayowezesha Sekta ya Nishati kuendeshwa kwa mafanikio ambayo yamepelekea leo hii tushuhudie hatua ikizidi kupigwa katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuokoa maisha ya watanzania na pia kuiwezesha Wizara ya Nishati kutatua changamoto zinazojitokeza lengo likiwa ni kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi.” Amesema Dkt. Biteko

Kuhusu mikataba hiyo ya Nishati Safi ya Kupikia, Dkt.Biteko ameiagiza REA na wadau kuhakikisha kuwa matokeo yanaonekana tena kwa uharaka akieleza kuwa “itakuwa aibu sana watanzania wanaona mikataba imesainiwa huku kukiwa hakuna matokeo, tusione kawaida kwa ndugu zetu kupoteza maisha kwa kutumia nishati isiyo safi, tuwaokoe kupitia miradi hii na tutumie kila fursa inayojitokeza.”

Amesisitiza kuwa, ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ni ya wote na inalenga kuokoa maisha ya watanzania hivyo hivyo iwe ni kipaumbele cha watu wote. 

Kuhusu usambazaji wa nishati vijijini ikiwemo umeme, ameipongeza Bodi ya REA kwa kusimamia ipasavyo miradi hiyo vijijini na kwa kuwahimiza wakandarasi kukamilisha kazi kwa wakati.

Akizungumzia jengo la REA alilolizindua, Dkt.Biteko amesema litawawezesha watumishi kutoa huduma kwa wananchi na kuwapongeza REA kwa kujenga jengo hilo la kisasa lenye ghorofa tano kwa gharama ya shilingi bilioni 9.8 kwa miezi 18 badala ya  shilingi bilioni 13 zilizopangwa awali.
Pamoja na kuipongeza REA kwa ujenzi wa jengo hilo la kisasa amewakumbusha kuwa, uwepo wa jengo wa jengo hilo lazima uende sambamba na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

“ Mimi naamini Jengo hili kweli ni muhimu lakini muhimu zaidi ni huduma kutoka kwenu kwenda kwa wananchi, kama tunasema kwamba tuna jengo zuri la ghorofa tano, halafu tukatoa huduma mbaya, jengo hili halitakuwa na maana yoyote hivyo uzuri wake uonekane kwenye huduma kuanzia sehemu ya mapokezi na wananchi watoke katika jengo hili wakiwa na furaha.” Amesisitiza Dkt. Biteko
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameagiza Watendaji wa Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa majengo ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake yanafungwa mfumo wa umeme jua ikiwa ni kuonesha kwa vitendo matumizi ya nishati safi yenye gharama nafuu.

kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe.Daniel  Sillo amesema tukio hilo ni alama ya ushirikiano kati ya REA na Taasisi za Jeshi ambapo amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za dhati katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, udhibiti wa rasilimali za misitu na kutengeneza fursa za ajira kupitia Nishati Safi ya Kupikia. 

Amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Dkt. Samia na  utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) kuwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 ziache matumizi ya kuni na mkaa na kuanza  kutumia vyanzo vya Nishati safi ya Kupikia ikwemo gesi asilia, umeme, bayogesi na makaa ya mawe yaliyoboreshwa.

Amesema kwa sasa nishati inayotumika kupikia chakula cha Wafungwa na Mahabusu  ni kuni kwa asilimia  98 ambapo Jeshi hilo lilianza kutekeleza Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kuanza kutumia nishati safi kupitia  gesi asilia na mkaa mbadala hivyo  kusainiwa kwa mkataba huo kutawezesha Jeshi la Magereza kutumia nishati safi ya kupikia kwenye magereza yake.

Amesema kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani itahakikisha fedha zilizotengwa pamoja vifaa kwenye programu hiyo zinasimamiwa ipasavyo ili lengo tarajiwa lifikiwe na hii ikienda sambamba na utoaji wa mafunzo  kwa watumishi wa Jeshi ili waweze kuisimamia na kutunza miundombinu itakayofungwa.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa pongezi kwa REA kwa kukamilisha jengo kubwa la kisasa ambalo linaifaharisha Dodoma  na pia amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kutoa sh.bilioni 214 kwa ajili ya shughuli za umeme mijini na vijijini ambapo mkoani Dodoma asilimia 92.2 ya vijiji  vimefikiwa na umeme huku kazi hiyo usambazaji umeme ikiendelea.

Pia amempongeza Rais, kwa miradi ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia uhamasishaji wa nishati hiyo na kueleza kuwa kasi ya kutumia nishati safi kwa wananchi inaongezeka.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alilolitoa wakati akizindua  mjadala wa kitaifa wa Nishati Safi ya kupikia na kutilia mkazo wakati akizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na kwamba Wizara ya Nishati ina wajibu wa kutekeleza agizo hilo na ndio maana taasisi yake ya REA  imesaini mikataba husika

Amesema Mikataba iliyosainiwa inahusisha masuala mbalimbali ikiwemo kufunga mifumo ya nishati safi  ya kupikia pamoja na usambazaji wa majiko na mitungi ya gesi  ipatayo laki nne ambayo inatolewa kwa bei ya ruzuku kwa wananchi hasa maeneo ya vijijini.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy alisema kuwa, Wakala huo kuhamia kwenye jengo lake kumewezesha kuokoa shilingi milioni 650 zilizokuwa zikitumika kwa mwaka kulipia kodi ya pango ambazo sasa zinaelekezwa kwenye maendeleo ya huduma zinazotolewa. 

Kuhusu mikataba ya Nishati Safi ya Kupikia alisema kwa upande wa Jeshi la Magereza,  mikataba iliyosainiwa ina thamani ya shilingi bilioni 35.23 ambapo kati ya fedha hizo 75.5% ambayo ni sawa na shilingi bilioni 26.57 zitatolewa na REA na 24.6% sawa na shilingi bilioni 8.66 zitatolewa na Jeshi hilo kwa mradi utakaotekelezwa kwa muda wa miaka mitatu katika Magereza 129 ya Tanzania Bara.

Mkataba wa Magereza unahusisha masuala mbalimbali ikiwemo ujenzi wa mifumo ya bayogesi (gesi vunde) 126, usimikaji wa mifumo 64 ya gesi ya LPG, usimikaji wa mfumo wa gesi asilia, usambazaji wa mitungi ya gesi (LPG) ya kilo 15 ikiwa na jiko la sahani mbili ipatayo 15,920 kwa watumishi wa Magereza na usambazaji wa tani 865 za mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe kutoka STAMICO.

Mhandisi saidy alisema kwa upande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mikataba iliyosainiwa ina thamani ya shilingi bilioni 5.75 ambapo kati ya fedha hizo asilimia 76 ambayo ni sawa na shilingi bilioni 4.37 itatolewa na REA na huku asilimia 24 sawa na shilingi bilioni 1.39 itatolewa na JKT.

Alisema fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi katika Kambi 22 za JKT kwa muda wa miaka miwili itakayohusisha ujenzi wa mitambo 9 ya bayogesi, majiko 291 ya kutumia mkaa mbadala (makaa ya mawe na tungamotaka), ujenzi wa mifumo 180 ya kupikia inayotumia LPG na sufuria zake, ununuzi wa tani 110 za mkaa unaotokana na makaa ya mawe, ununuzi wa mashine 60 za kutengeneza mkaa mbadala na mafunzo kwa vijana wapatao 50,000.

Wadau wengine waliosaini mikataba ya Nishati Safi ya Kupikia ni kampuni zinazofanya biashara ya gesi ya mitungi ikiwemo Taifa Gas, Manjis, Oryx pamoja na Lake Oil ambapo wanasambaza mitungi ya gesi ya kupikia ipatayo 452,445  kwa bei ya ruzuku katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Posted by MROKI On Friday, September 13, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo