Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza
na viongozi, waumini na wananchi mbalimbali wakati wa kilele cha Sherehe za
Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Kanisa la New Life Outreach Tanzania
iliyofanyika katika kanisa hilo eneo la Sakina mkoani Arusha tarehe 07 Septemba
2024.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai
kwa viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Ofisi ya Msajili wa
Jumuiya, kusimamia kikamilifu Sheria ya Usajili wa Jumuiya pamoja na kanuni
zake ili kuhakikisha kuwa Taasisi zinazosajiliwa zikiwemo za kidini
zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia malengo na masharti ya usajili wake.
Makamu
wa Rais ametoa rai hiyo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Maadhimisho ya Jubilei
ya Miaka 50 ya Kanisa la New Life Outreach iliyofanyika katika kanisa hilo
Sakina mkoani Arusha. Amesema hivi sasa yameibuka mafundisho ya baadhi ya
viongozi wa dini yanayowaaminisha wafuasi wao kutegemea miujiza zaidi ili
kupata maendeleo badala ya kufanya kazi kwa bidii.
Ameongeza
kwamba imeshuhudiwa kuongezeka kwa
wahubiri wanaojilimbikizia fedha na mali binafsi kutokana na sadaka na mauzo ya
vitu mbalimbali na wengi wa wahanga wa mahubiri ya aina hiyo ni wananchi
wanaokabiliwa na shida au matatizo mbalimbali ya maisha.
Makamu
wa Rais amewasihi viongozi wa dini kuungana na serikali kukemea vikali
mafundisho na matendo hayo yasiyofaa katika jamii na yasiyozingatia sheria za
nchi. Pia ametoa wito kwa viongozi wote kuwahimiza
wananchi kufanya kazi kwa bidii, maarifa na uzalendo, huku wakimuomba Mwenyezi
Mungu abariki kazi zao.
Halikadhalika
Makamu wa Rais amesema hivi sasa kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii
hali inayopelekewa na matumizi holela ya mitandao ya kijamii, ambapo wananchi
hususan vijana wengi wanadhani ili kuwa kijana wa kisasa, inawalazimu kuiga
mambo yanayooneshwa kwenye mitandao hiyo yakiwemo yale yasiyo endana na mila na
desturi.
Amesema
kukosekana kwa hofu ya Mungu katika jamii kunapelekea kuongezeka kwa matukio ya mauaji ya kikatili,
ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto na wanawake, familia za mzazi
mmoja, watoto waliozaliwa nje ya ndoa, migogoro ya ndoa, talaka, migogoro ya
mirathi na ardhi, ubadhirifu wa mali za umma na matukio ya watu kujinyonga.
Aidha
Makamu wa Rais amekemea tabia za uzembe na kutozingatia sheria za usalama
barabarani ambazo zimepelekea kushamiri kwa ajali mbaya za barabarani
zinazogharimu maisha ya wananchi wengi.
Ametoa
rai kwa wakaguzi wa magari wa LATRA na Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani
kutimiza wajibu wao ili kudhibiti magari mabovu yasiingie barabarani na
kuhakikisha vidhibiti mwendo vinafanya kazi, pamoja na kukagua sifa za madereva
hasa wa mabasi ya abiria na malori. Ameongeza kwamba wamiliki wa Mabasi na
Malori wanapaswa kuhakikisha magari yao yanakuwa na madereva walau 2 kwa safari
zote ndefu zinazozidi kilomita 300. Vilevile ameagiza Wakala ya Barabara Nchini
(TANROADS) kuhakikisha alama za tahadhari zinawekwa katika maeneo yote
hatarishi ya barabara kuu.
Makamu
wa Rais ametoa wito kwa wasafiri wote
nchini kuzingatia kufunga mikanda wakati
wote wa safari na kutoa taarifa kwa Kikosi cha Usalama Barabarani pale dereva
wa chombo wanachosafiria anapoendesha kwa mwendo mkali kupita kiasi.
Pia
Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla kushirikiana na serikali katika kukabiliana
na athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Amesema uhai wa
wanadamu katika dunia unatishiwa na uharibifu wa mazingira ambao umekithiri
ambapo pamoja na jitihada mbalimbali za kitaifa na kimataifa zinazochukuliwa
kukabiliana na hali hiyo, lakini bado
matokeo yake si ya kuridhisha. Ameongeza kwamba uharibifu wa misitu na ukataji
wa miti unaonekana katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo mkoani Arusha.
Makamu
wa Rais amesema Serikali itaendelea kuenzi mchango mkubwa wa madhehebu ya Dini,
katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii na itaendelea kusimamia na
kulinda haki ya kuabudu kwa wananchi wote kwa mujibu wa ibara ya 19 (2) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwamba wananchi wanaendelea
kuishi katika mazingira ya haki na amani.
Kwa
upande wake Muasisi wa Kanisa la New Life Outreach Tanzania Mwinjilisti Dkt.
Egon Falk ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa
kibali cha kuhubiri neno la Mungu kwa miaka 50.
Amesema Kanisa hilo litaendelea kufuata sheria na taratibu za nchi wakati wa utoaji wa huduma ya kuhubiri neno la Mungu na huduma nyingine za kijamii. Kanisa hilo linamiliki Shule mbili za msingi na moja ya sekondari ambazo zimekuwa zikitoa ufadhili wa masomo kwa watoto wanaopitia mazingira magumu ya Maisha.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akishiriki
kilele cha Sherehe za Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Kanisa la New Life
Outreach Tanzania iliyofanyika katika kanisa hilo eneo la Sakina mkoani Arusha
tarehe 07 Septemba 2024.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na
viongozi mbalimbali katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi New
Life inayomilika na Kanisa la New Life Outreach Tanzania mara baada ya
kushiriki kilele cha Sherehe za Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Kanisa la
New Life Outreach Tanzania iliyofanyika katika kanisa hilo eneo la Sakina
mkoani Arusha tarehe 07 Septemba 2024.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango na Mkewe
Mama Mbonimpaye Mpango wakikabidhiwa zawadi ya Biblia Takatifu kutoka kwa Muasisi
wa Kanisa la New Life Outreach Tanzania Mwinjilisti Dkt. Egon Falk na Mkewe Bi.
Hanna Falk mara baada ya kushiriki kilele cha Sherehe za Maadhimisho ya Jubilei
ya Miaka 50 ya Kanisa la New Life Outreach Tanzania iliyofanyika katika kanisa
hilo eneo la Sakina mkoani Arusha tarehe 07 Septemba 2024.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwakabidhi
tuzo Muasisi wa Kanisa la New Life Outreach Tanzania Mwinjilisti Dkt. Egon Falk
na Mkewe Bi. Hanna Falk kwa kusimamia vema kanisa hilo kwa miaka 50 wakati wa kilele
cha Sherehe za Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Kanisa la New Life
Outreach Tanzania iliyofanyika katika kanisa hilo eneo la Sakina mkoani Arusha
tarehe 07 Septemba 2024.
0 comments:
Post a Comment