Tume ya Madini leo Agosti 04, 2024 imeendelea kutoa elimu kwa wadau wa madini katika Maonesho ya Nane Nane yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma
Elimu imetolewa katika maeneo ya usimamizi/udhibiti wa Sekta ya Madini na ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na tozo mbalimbali zinazotokana na shughuli za madini, utoaji na usimamizi wa leseni za utafutaji wa madini, uchimbaji na biashara ya madini pamoja na namna ya kujisajili katika mfumo wa Online Mining Cadastre Transaction Portal (OMCTP), ukaguzi na usalama wa migodi, afya, mazingira na njia bora ya uzalishaji wa madini kwa migodi midogo, ya kati na mikubwa.
Maeneo mengine ni pamoja na usimamizi wa biashara ya madini inayofanyika katika masoko ya madini yaliyoanzishwa nchini, ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini na wajibu wa wawekezaji kwa jamii katika uboreshaji wa huduma (Corporate Social Responsibity; CSR)
Aidha, elimu imelenga katika maeneo ya upatikanaji wa vibali mbalimbali vya kusafirisha madini ndani na nje ya nchi na huduma zinazotolewa na Maabara ya Tume ya Madini hususan upimaji wa madini ya metali.
Wakizungumza wadau mbalimbali waliotembelea banda la Tume ya Madini wamepongeza kazi kubwa inayofanywa na Tume kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini kupitia utoaji na usimamizi wa leseni za madini, usimamizi wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini, usimamizi wa usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini.
Katika hatua nyingine, wadau wa madini wamekoshwa na bidhaa za uchimbaji na vifaa kinga sambamba na elimu kutoka kwa kampuni ya Kidee Mining (T) Limited.
Akielezea shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo mmiliki wake, Fey Hassan Kidee amesema kuwa lengo la uanzishwaji wa kampuni ni kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini kuchimba madini kwa kutokuharibu mazingira na usalama migodini kwa kuwauzia vifaa ambavyo vina ubora wa hali ya juu vyenye kurahisisha utoaji wa udongo ndani ya mgodi kwa haraka zaidi.
0 comments:
Post a Comment