Nafasi Ya Matangazo

August 05, 2024
















Naibu Waziri Mkuu Dotto Biteko amewaagiza Maafisa ugani kote nchini kuhakikisha wanatoa elimu bora na stahiki kwa Wafugaji, Wakulima na Wavuvi kama hatua ya kuongeza tija ya uzalishaji katika sekta hizo kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya masoko ya ndani na la Kimataifa.

Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati ametoa kauli hiyo Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego (5-Aug-2024 ) katika ufunguzi wa mashindano ya paredi ya mifugo mbalimbali katika Maonesho ya Kimataifa ya Nane nane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa paredi ya mifugo huchangia kuhamasisha,kukuza na kuendeleza ufugaji bora katika kuchangia katika maendeleo ya Taifa na Mtu Mmoja Mmoja.

“Mifugo ni utajiri fugeni kisasa mtaona matunda yake haraka,” Amesisitiza Biteko 

Amesema ufugaji wenye tija kwa kutumia teknolojia na mbinu za kisasa utasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi hasa wafugaji, wakulima na wavuvi kuongeza vipato vya maradufu na kuchangia pato la taifa kwa kiwango kikubwa.

Biteko ameeleza kuwa mafanikio hayo yatafikiwa iwapo tu Maafisa ugani kote nchini watawajibika ipasavyo katika utoaji wa elimu ya ufugaji wa kibiashara utakaosaidia kukidhi mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wao, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti na Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde wamewahakikishia wananchi kuwa Serikali inaendelea kuweka mipango na mikakati madhubuti ili kuhakikisha sekta hizo zinaongeza tija katika uzalishaji kama hatua ya kuwaondoa wananchi na umaskini wa kipato.

Mashindano ya Paredi ya Mifugo yamekuwa kivutia kikubwa kwa wananchi kwa sababu hujumuisha mifugo bora yenye umri mdogo kati ya miaka Mitatu hadi Minne ambayo imefugwa kisasa kwa kuwa na kilo kati ya 700 hadi 800 pamoja na ngombe wanaotoa maziwa mengi. 

Kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na zaidi ya ng’ombe milioni 37, Mbuzi milioni 27.6,Kondoo milioni 9.4 na Kuku milioni 103.


Picha za matukio mbalimbali ya maonesho ya paredi za mifugo katika maonesho ya kimataifa ya Nanenane Jijini Dodoma.
Posted by MROKI On Monday, August 05, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo