Nafasi Ya Matangazo

June 23, 2024








🔴Azindua mifumo minne ya kidijiti Serikalini 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka taasisi za umma ziweke mipango madhubuti ya kutumia mifumo ya kidijitali ambayo italeta mageuzi ya kiutendaji na kuifanya Tanzania kuendana na mapinduzi ya nne ya viwanda yanayotumia TEHAMA.

Amesema kuwa mifumo hiyo pamoja na mambo mengine itasaidia kuwabana watumishi wazembe. “Kunahitajika msukumo kuhakikisha mifumo hii inatumika. Niwaelekeze Watendaji Wakuu na watumishi wa umma kuhakikisha mnaandaa mipango na mikakati ya muda mfupi na mrefu ya jinsi mifumo ya kidigitali itakavyotumika kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.”

Amesema hayo leo (Jumapili, Juni 23, 2024) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma. Pia alizindua Mifumo ya Kidijitali ya Uwajibikaji na Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma iliyosanifiwa na kujengwa na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora.

Mifumo iliyozinduliwa ni Mfumo Jumuishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (e-WATUMISHI), Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi (PEPMIS kwa watumishi wa umma na PIPMIS kwa taasisi za umma), Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma (HR Assessment) na Mfumo wa e-Mrejesho.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaelekeza watendaji wakuu na watumishi wa umma waandae mipango inayopimika. “Mipango hii inapaswa kuwa wazi, yenye malengo yanayopimika na kuzingatia mahitaji ya wananchi na matakwa ya sera za Serikali.”

Katika hatua nyingine, Majaliwa amezitaka taasisi za umma kutoa mafunzo na kuhamasisha matumizi sahihi ya mifumo kwa watumishi wote kwa kuwa ni mipya kwa watumiaji wengi. Ni muhimu kuhamasisha na kuwaelimisha watumishi kuhusu umuhimu wa mifumo hii katika kuboresha huduma kwa umma na kufikia malengo ya Serikali.”

Mapema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alisema ubunifu wa mifumo hiyo iliyosanifiwa na kujengwa na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora umeokoa zaidi ya sh. bilioni 11 ambazo zingetumika kununua mifumo mipya na sh. milioni 616 ambazo zingetumika kila mwka kulipia leseni za mifumo hiyo.

“Mifumo ambayo imekamilika na inasomana, imejengwa na vija25 wa Kitanzania kutoka Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Ofisi ya Rais – Ikulu, Wizara ya Fedha, Wakala wa Serikali Mtandao, Ofisi ya Rais – TAMISEMI na PSRS,” alisema.

Vijana walikabidhiwa vyeti na kutunukiwa tuzo maalumu ili kutambua mchango wao kwa Taifa.
Posted by MROKI On Sunday, June 23, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo