Na Happiness Shayo-Dodoma
Waziri wa Maliasili
na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema kuwa katika kuhakikisha
kunakuwapo na vyanzo endelevu vya uzalishaji wa mbegu bora za miti sambamba na
ulimaji miti hiyo kibiashara, Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) imeanzisha upandaji wa miti jamii ya Mninga katika mashamba yake
ya Miti ya Ruvu lililoko Kibaha – Pwani, Mpepo lililoko Nyasa – Ruvuma na
Shamba la Mbegu za miti Kising’a lililoko Mkoa wa Iringa.
Ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Sikonge,
Mhe. Joseph George Kakunda aliyetaka kujua lini Serikali itazalisha mbegu za Mti wa Mninga ili
kufanya mti huo kuwa zao la kibiashara.
Ameongeza kuwa
Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imefanikiwa
kuzalisha na kugawa kwa wadau mbalimbali jumla ya miche ya mninga 5,115
kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024.
’’Kwa Mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia TFS
ilikusanya jumla ya kilo 237 za mbegu za Mninga kutoka katika vyanzo mbalimbali
na ilifanikiwa kuzalisha na kugawa kwa
wadau mbalimbali jumla ya miche ya mninga 5,115”
alisisitiza.
Amesema pamoja na
jitihada hizo, Serikali imejizatiti kuongeza ukusanyaji wa mbegu, kuotesha na
kusambaza mbegu bora na miche ya Mninga kwa wadau mbalimbali kupitia vituo
vyake vya uzalishaji mbegu za miti.
Aidha, amesema
Serikali itaendelea kuhamasisha taasisi za sekta binafsi pamoja na muungano wa
wananchi kupitia vyama mbalimbali vya wakulima wa miti ili waweze kupanda miti
hiyo ambayo inaweza kuwa adimu na kutoweka badala ya kupoteza fedha kuagiza
mbegu za miche kutoka nchi za jirani kama Zimbabwe.
Katika hatua
nyingine, Waziri Kairuki ameweka bayana kuwa Tanzania imekuwa ikipokea wageni kutoka
nchi za jirani wakija kujifunza kuhusu upandaji miti na hivyo Serikali itajitosheleza
katika mbegu hizo za miti bora ambayo imeanza kupotea kwa mahitaji ya ndani na
kuuza nje ili kupata fedha za kigeni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment