Nafasi Ya Matangazo

June 28, 2024



Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam 
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Makandarasi nchini kutekeleza miradi ya ujenzi kwa ubora na uzalendo mkubwa ili wainue uchumi wa nchi na kuhakikisha unashikiliwa na Makandarasi wazawa.

Dkt. Biteko ameyasema hayo tarehe 28 Juni, 2024 alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kufunga Kongamano la Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi lililoandaliwa na Chama cha Umoja wa Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi Tanzania (TUCASA) jijini Dar es Salaam.

Vile vile, amewataka kuheshimu matumizi ya fedha za miradi, kwa kufanyia shughuli za ujenzi, na faida watakayoipata kuiwekeza na kutunza kampuni zao.

Aidha, ameielekeza Wizara ya Ujenzi kuweka mkakati wa kuwainua makandarasi nchini na kuhakikisha unatekelezwa ipasavyo kuanzia ngazi ya Wizara ya Ujenzi yenyewe pamoja na Wizara ya Fedha kisha kuendelea na mazungumzo na mabenki ili kuja na mpango mzuri wa kuwawezesha makandarasi kimtaji.

Amesema Ofisi ya Waziri Mkuu itaelekeza sekta zingine zikiwemo Nishati, Maji, Uchukuzi, kuhakikisha zina wabeba wakandarasi wazawa; pamoja na kuziwekea malengo ambayo kila mwaka kwenye mkutano wa makandarasi unapima utekelezaji wa malengo hayo.

Aidha, amewataka kuiga mfano kutoka Wizara ya Kilimo ya BBT, Wizara ya Ujenzi iwasaidie vijana kuanzisha makampuni na kuwapatia kazi ndogo ndogo ili kuwajengea uzoefu.

Dkt. Biteko pia amesisitiza kuwa, Serikali imeendelea kuwachukulia hatua watumishi wote wa umma wanaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa. 

"Napenda niwahakikishie kuwa Serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU itaendelea kuchukua hatua za kisheria kwa watumishi wanaojihusisha na rushwa. Ombi langu kwenu, pale mnapokumbana na tatizo la rushwa msisite kutoa taarifa TAKUKURU," amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko amesema, katika  mpango mkakati wa kukuza makandarasi wa ndani, kumewekwa kipangele cha kuhakikisha kuwa miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za mikopo kutoka kwa wadau wa maendeleo kunatengwa asilimia isiyopungua 20 kwa ajili ya makandarasi wa ndani.

Dhamira ya Mhe Rais ni kuwajengea uwezo makandarasi wazawa na ametoa maelekezo kwa viongozi wote wa Serikali pamoja na watumishi wa ngazi zote kuhahakikisha wanatekeleza agizo lake la kuwakuza na kuwajengea uwezo wakandarasi wa ndani ili waweze kutekeleza miradi mikubwa.

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa amesema Rais Samia anatambua mchango wa wakandarasi wazawa nchini ili wawe mstari wa mbele katika ujenzi na maendeleo ya nchi na kusisitiza kuwa wakandarasi wazawa wameendelea  kuetekeleza miradi mbalimbali nchini.

Naye, Mwenyekiti wa TUCASA Samwel Marwa, ameiomba Serikali iwe mlezi kwa TUCASA ili kuwajengea uwezo wa kufanya kazi na kusimama wenyewe. Pia ameiomba  Serikali kuendelea kupambana na rushwa ili kuifanya TUCASA kufanya kazi kwa weledi na kupata faida katika majukumu yao.
Posted by MROKI On Friday, June 28, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo