Nafasi Ya Matangazo

June 28, 2024

Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akizungumza kwenye kikao Maalum cha kujadili hoja za CAG katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mkalama.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkalama James Mkwega akizungumza wakati akifungua Kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mkalama kwa ajili ya kujadili hoja za CAG.
Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga akitoa maelekezo ya Serikali kwa Watendaji wa Halmashauri ya Mkalama kuhusu namna ya kupunguza hoja za CAG pamoja na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo.


Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mkalama.
kikiendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego, ameonya kuwa hatapenda kusikia miradi yoyote ya maendeleo inayoibuliwa katika Halmashauri za mkoa huo inakwama kwa kisingizio cha kutaka kuongezewa fedha za ziada.

Mkuu huyo wa mkoa wa Singida ametoa kauli hiyo (28 Juni, 2024) katika Kikao Maalum cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mkalama cha kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.

Rc Dendego amesema mpaka sasa mkoa wa Singida una miradi 724 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 31 ambayo ujenzi wake umekwama kutokana na miradi hiyo kuhitaji fedha za ziada. 

Amesisitiza kuwa kuanzia sasa Halmashauri zote zinatakiwa kuhakikisha zinakamilisha miradi iliyopo kwanza ikiwemo maboma yote yaliyojengwa kabla ya kuanzisha miradi mipya.

Aidha, Rc Dendego pia amewaagiza Madiwani kuwa mstari wa mbele katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo badala ya wao nao kuanza kulalamika kuwa miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao haikamiliki.

“Madiwani mnatakiwa kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo kwenye maeneo yenu na miradi hiyo ilete matokeo chanya kulingana na thamani ya fedha”, Amesisitiza Dendego.

Naye,Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri mkoani humo kuwa wabunifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo kuajiri kwa mkataba Wahandisi waliostaafu na mafundi wenye ujuzi wa kujenga ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.

Dkt. Mganga amesema anajua uhaba wa Watumishi hasa kwenye kada ya Uhandisi lakini isiwe ndio kisingizio cha miradi kukwama hivyo ni muhimu Wakurugenzi wakawa na njia mbadala ya kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na kuzingatia ubora unaotakiwa.

Amesisitiza kuwa miradi yote ya maendeleo ambayo bado haijakamika lazima iingizwe kwenye bajeti mpya ili ujenzi wake uweze kukamilika. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkalama James Mkwega, amemshuruku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuipatia fedha nyingi Halmashauri hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mkwega amesema tangu aanze kazi ya udiwani hajawahi kuona fedha nyingi zinazotolewa na Serikali kama kipindi hiki hivyo wao kama Madiwani wanajukumu kubwa la kuhakikisha miradi inayoteelezwa kwenye maeneo yao inakuwa bora kulingana na thamani ya fedha.


Imetolewa na 
Kitengo cha Mawasiliano
Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Singida.
0755 516 591
0712 762071
PTC 1. 
PTC 2. 
PTC 3. 
PTC 4. 
PTC 5. 
Posted by MROKI On Friday, June 28, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo