Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inakaribisha maombi kutoka taasisi na asasi za kiraia nchini zenye nia ya kutoa elimu ya mpiga kura katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura 2024, unaotarajiwa kuanza tarehe 1 Julai, 2024 katika Mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora.
Mwaliko huo umetolewa kupitia tangazo la leo tarehe 17 Mei, 20224 lililosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Kailima, R. K kwa mujibu wa kifungu cha 10(1)(g) na (h) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024, kinachoipa wajibu Tume kutoa elimu ya mpiga kura nchini, kuratibu na kusimamia taasisi na asasi za kiraia zinazotoa elimu hiyo.
Kwa mujibu wa tangazo la mwaliko taasisi na asasi za kiraia zenye nia ya kutoa elimu ya mpiga kura zinatakiwa kuwasilisha maombi yao katika mfumo wa kusajili watazamaji, asasi za kiraia na vyombo vya habari (Accreditation Management System - AMS) unaopatikana katika anwani ya https://ams.inec.go.tz
Tangazo hilo linafafanua kuwa maombi ya kutoa elimu yanapokelewa kuanzia leo tarehe 17 hadi 30 Mei, 2024 na taasisi au asasi ya kiraia yenye nia ya kutoa elimu ya mpiga kura inatakiwa kukidhi vigezo vifuatavyo:-
- iwe imesajiliwa kwa mujibu wa Sheria za Tanzania;
- iwe imetuma maombi kupitia mfumo wa Accreditation Management System (AMS) kupitia anwani ya https://ams.inec.go.tz
- iwe imefanya kazi nchini kwa kipindi kisichopungua miezi sita tangu kusajiliwa kwake;
- ikiwa taasisi au asasi ya kiraia inahusisha watendaji wa kimataifa, miongoni mwa watendaji wake wakuu, wawili ambao taarifa zao zitawasilishwa wanapaswa wawe Watanzania;
- katika utendaji wake, iwe haijahusishwa na uchochezi au kuvuruga amani;
- iwe na uzoefu wa kutoa elimu ya mpiga kura; na
- iwe tayari kujigharamia katika kutoa elimu ya mpiga kura.
Aidha, taasisi au asasi ya kiraia itakapowasilisha maombi katika mfumo, inatakiwa kutekeleza yafuatayo:-
- kuambatisha nakala au kivuli cha cheti cha usajili;
- kuambatisha nakala au kivuli cha katiba ya taasisi au asasi husika;
- kujaza majina matatu ya viongozi wa juu wa taasisi au asasi husika;
- kujaza anwani kamili ya makazi na namba za simu za ofisi na za viongozi wake;
- kuainisha vyanzo vya fedha zitakazotumika katika utelekelezaji wa jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura;
- kuambatisha ratiba itakayoonesha tarehe na mahali elimu ya mpiga kura itakapotolewa katika halmashauri husika; na
- kuorodhesha katika mfumo watendaji watakaotoa elimu ya mpiga kura walioteuliwa na taasisi au asasi iliyopewa kibali.
Tume haitahusika na utoaji wa rasilimali fedha au rasilimali nyingine kwa ajili ya kugharamia zoezi la utoaji wa elimu ya mpiga kura kwa taasisi au asasi za kiraia zitakazopewa kibali.
0 comments:
Post a Comment