Nafasi Ya Matangazo

May 18, 2024










Na Mwandishi wetu
Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo, amekabidhi magari mawili, moja la kubebea Wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya iliyopo kata ya Mwada tarafa ya Mbugwe na lingine kwa ajili usimamizi huduma za Afya kwenye Vituo yenye thamani ya shilingi milioni 400.

Akikabidhi magari hayo Mei 18 2024 katika hafla iliyofanyika Kijiji cha Mwada, Mhe. Sillo ameitaka Halmashauri ikayasimamie magari hayo ili yakatoe huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.

“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapenda sana ndio maana ametoa magari haya yakatoe huduma ya kubebea Wagonjwa na kuwapeleka kwenye huduma kwa haraka" Alisema Sillo 

Mhe. Sillo alisema Serikali imeendelea kuboresha sekta ya afya ambapo imejenga Hospitali ya Wilaya ya Babati kwa zaidi ya shilingi bilioni 3.326, vituo vya afya kata ya Madunga, Bashnet, Ayasanda na Gidas kwa shilingi Bilioni 1.75 na kwa sasa zinasubiriwa milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Kata ya Kiru na kwamba shilingi milioni 450 zimetolewa kwenye zahanati tisa.

Awali akizungumza Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Dkt. Hosea Madama alisema kabla ya gari hilo, walikuwa wakitumia gari dogo aina ya Suzuki Marut moja ambalo lipo Kituo cha Afya Magugu, hivyo wanamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mbunge kwa kuhakikisha magari hayo yanapatikana.

Alisema kwa sasa wamepata magari mawili ya kubebea Wagonjwa, moja limeshakabidhiwa tarafa ya Bashnet na kwa sasa uhitaji zaidi ni tarafa ya Ghorowa na Babati.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Babati Mheshimiwa Jackson Haibey, alisema magari hayo yatakuwa msaada mkubwa kwa Wananchi hivyo yatumike kama ilivyokusudiwa.

Alisema ni heshima kubwa kuwa na Mbunge anayekubalika na watu na kuaminika na Serikali na ndio maana kapewa nafasi ya kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Aidha, hafla hiyo ilihudhuriwa na Mbunge wa Viti Maalum kundi la Vijana Taifa Mhe. Asia Halamga Viongozi mbalimbali wa Chama, Serikali na Wananchi.
Posted by MROKI On Saturday, May 18, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo