Kuanzia Aprili 1,2024 hadi
Aprili 7,2024 watu 15 wamefariki dunia kutokana na kusombwa na maji ya mvua
zinazoendelea kunyesha, wengine wakiwa wanaogelea, wengine wakiwa wanavuka
maeneo ambayo maji yanatiririka kwa kasi na wengine kutokana na kutumbukia
kwenye mashimo/madimbwi yaliyojaa maji. Miongoni mwa watu hao watoto ni 12 na
watu wazima ni 3.
Matukio hayo yametokea katika
Wilaya mbalimbali hapa nchini. Wilaya ya Kalambo Mkoa wa Rukwa mtu mmoja
mwanaume miaka 18, alisombwa na maji ya mvua yaliyokuwa yakitokea milimani
wakati akijaribu kuvuka daraja Aprili 1,2024.
Tarehe hiyo hiyo katika Wilaya ya
Kilwa Mkoa wa Lindi watoto 2 wote wakiwa na miaka 12 walikufa maji baada ya
kusombwa na maji ya mvua.
Aprili 2,2024 mwanaume mmoja
wa miaka 28, huko katika Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe alikufa baada ya
kufukiwa na udongo ulioporomoka kutokana na mvua kubwa zilizokuwa zinanyesha.
Aprili 3,2024 huko Wilayani
Muheza Mkoa wa Tanga, mtoto wa miaka 8 alikufa maji wakati akiogelea.
Mkoani Pwani Aprili 3,2024
Wilaya ya Mkuranga mtoto mmoja wa miaka 10 alifariki Dunia akiogelea mto Mzinga
na Wilaya ya Kibaha mtoto wa miaka 12 alikufa maji yaliyokuwa yamejaa katika
bonde la mpunga.
Aprili 5,2024 mwanamke mmoja
mwenye umri wa miaka 55 huko Wilayani Babati moani Manyara alikufa maji baada
ya kutumbukia kwenye shimo lenye maji.
Aidha, Aprili 7,2024 huko
katika Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya watoto 5 wenye umri kati ya miaka 5 na 6
walifariki dunia baada ya kuzama kwenye dimbwi lilojaa maji ya mvua wakiwa
wanaogelea.
Pia tarehe hiyo hiyo huko Mkoani Geita watoto 2 wenye umri wa miaka
9 na 14 walifariki dunia baada ya kusombwa na maji ya mvua yaliyokuwa
yanatiririka kutoka milimani wakitoka kuokota kuni.
Jeshi la Polisi kutokana na
mtiririko wa matukio haya kwa mwezi huu na katika kipindi kifupi na
uzoefu wa matukio mengine kama haya ya siku za nyuma linaendelea kutoa wito na
tahadhari kwa watu wote hususani wazazi na walezi kuwalinda watoto kwa karibu
sana na kuwapa maelekezo sahihi kutokana na mvua hizi zinazoendelea kunyesha.
Pia Viongozi wa Serikali za Mitaa, Waalimu mashuleni, Viongozi wa Dini
tuendelee kuelimisha watoto wetu kujihadhari na maji yaliyotuama au
yanayotembea na wala wasishindane na maji ya mvua yanayotiririka kwani ni
hatari kwa maisha yao. Kila mmoja wetu kwa nafasi yake akemee anapoona watoto
wakicheza, wakipita au kuogelea kwenye maeneo hatarishi.
Sehemu ambazo
zinastahili kuwekwa alama za tahadhari ziwekwe au kufunikwa mfano mashimo
yaliyochimbwa kwa ajili ya visima vya maji majumbani na sehemu zingine.
0 comments:
Post a Comment