Nafasi Ya Matangazo

March 19, 2024







Wakuu wa Shule za msingi Mkoa wa Dodoma, wametakiwa kuweka utaratibu kwa wanafunzi kukimbia mchaka mchaka asubuhi kabla ya masomo kwani zoezi hili lina faida nyingi ikiwemo kuimarisha afya ya akili, ukakamavu pamoja na uzalendo kupitia nyimbo zinazoimbwa wakati wa zoezi hilo.

Hayo yamebainishwa leo Machi 19, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule wakati wa uzinduzi wa Juma la wadau wa Elimu Mkoa wa Dodoma hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari Dodoma iliyopo Jijini humo.

"Kupitia Juma hili, tutadhihirisha Dodoma tumeamua kufanya Mapinduzi kwenye Elimu. Nitoe maelekezo hapa, shule zote ziweke utaratibu kwa wanafunzi kukimbia mchaka mchaka kwani zoezi hili lina faida kubwa kwao kama vile kuimarisha afya ya akili, ukakamavu kupitia kukimbia pamoja na uzalendo kutoka na zile nyimbo zinazoimbwa" Amesema Mhe. Senyamule

Kadhalika, Mkuu wa Mkoa amezungumzia umuhimu wa michezo kwani Juma hili linakwenda sambamba na Bonanza la michezo mbalimbali kuelekea kilele chake Machi 24, 2024.

"Shirikisho la michezo Tanzania TFF limetoka mipira 1,000 ambayo nitaigawa leo kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma. Tutafuatilia kuhakikisha Mipira hii inatumika na sio kuwekea kabatini. Michezo ni afya kwani asilimia 30 ya wananchi wanakabiliwa na magonjwa yasiyoambukiza kutokana na kukosa kushiriki michezo." Amesisitiza Mhe. Senyamule.

Naye Afisa Elimu Mkoa wa Dodoma Mwl. Vicent Kayombo, amesema Juma hili ni matokeo ya maagizo ya Mhe. Senyamule kwa wakuu wa Shule zote za Mkoa wa Dodoma kufanya vikao na wadau wa Elimu pamoja na wazazi ikiwa ni mkakati wa kuinua taaluma ambao pia umesaidia kupatikana kwa kauli mbiu ya Mkoa ambayo ni "Uwajibikaji wangu, ndio msingi wa kuinua ubora wa Elimu na ufaulu Dodoma" ambayo ndio inatumika pia kwenye Juma hilo.
Posted by MROKI On Tuesday, March 19, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo