Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akitazama mchoro wa mradi wa umeme wa Rumakali utakaozalisha megawati 222 wilayani Makete mkoani Njombe tarehe 22 Februari 2024.
Sehemu ya Mto Rumakali ambayo maporomoko yake ya maji yatazalisha umeme wa megawati 222 wilayani Makete mkoani Njombe. ****************
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, mradi wa umeme wa maji wa
Rumakali utakaozalisha megawati 222 uliopo wilayani Makete mkoani Njombe sasa
unaanza kutekelezwa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa, vyanzo vyote vya umeme
sasa viendelezwe.
Dkt. Biteko amesema hayo
tarehe 22 Februari 2024 wilayani Makete mkoani Njombe mara baada ya kutembelea
eneo lenye maporomoko ya maji ya Mto Rumakali ambapo tuta la kuzuia maji yatakayozalisha
umeme litajengwa pamoja na mitambo ya kuzalisha umeme
"Upembuzi yakinifu wa
mradi huu ulifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1998 na uhuishaji wake ukafanyika
mwaka 2022 ambao ulionesha kuwa mradi unatekelezeka na una manufaa ya kiuchumi
na kijamii hivyo maagizo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuanza kuutekeleza ili
kuongeza vyanzo vya umeme." Amesema Dkt. Biteko
Amesema kuwa, pamoja na
utekelezaji wa mradi wa umeme Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha megawati
2115 lakini maendeleo makubwa yanayoendelea kutokea katika nchi yatahitaji
umeme mwingi na hivyo Serikali inapata msukumo wa kuendeleza vyanzo vingine vya
umeme ikiwemo mradi huo wa Rumakali.
Ameeleza kuwa, hatua
inayofuata kwenye mradi huo ni utafutaji wa mjenzi ambaye atapatikana kwa njia
ya ushindani wa tenda.
Amesema kuwa, mradi huo ni
mkubwa na wa kielelezo kwani utatoa umeme mwingi kuliko miradi mingine ya umeme
wa maji iliyopo nchini kama vile Kidatu, Kihansi, Mtera, Hale, Nyumba ya Mungu,
Pangani na Rusumo hivyo Serikali imeamua kwa dhati kuutekeleza.
Ameeleza kuwa, mradi mwingine
mkubwa wa maji unaoenda kutekelezwa ni mradi wa Ruhudji utakaozalisha megawati
358 uliopo mkoani Njombe na kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kutunza
mazingira ambayo ndiyo yatakayopelekea uwepo wa maji ya kutosha muda wote ili
kuzalisha umeme.
Ametanabaisha kuwa, vyanzo
vingine mbadala vya umeme ambavyo vitaendelezwa ni pamoja na Upepo
akitolea mfano mradi wa Makambako utakaozalisha megawati 600 na mradi wa umeme
Jua ambao umeanza kutekelezwa wilayani Kishapu na utazalisha megawati 150.
Amesema kuwa, nia ya Serikali
ni kuondoa kadhia ya kutopata umeme wa uhakika ambayo wananchi wamekuwa
wakiipata ambayo inatokana na kutegemea vyanzo vichache vya uzalishaji umeme
ambavyo ni Maji na Gesi Asilia.
Katika hatua nyingine, Dkt.
Biteko amewapongeza wananchi katika Wilaya ya Makete kwa utunzaji wa mazingira
ambao umepelekea mto Rumakali kuwa na maporomoko ya maji ya kutosha kuweza
kuzalisha umeme.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa
wa Njombe, Anthony Mtaka amesema kuwa, moja ya vipaumbele vya Mkoa huo ni
utunzaji wa mazingira hivyo wamezielekeza Mamlaka za Serikali za mitaa kuweka
mkazo kwenye usimamizi wa sheria ya mazingira hususani kwenye vyanzo vya maji
na kuwaelekeza wananchi shughuli gani zifanyike na zisifanyike ili kutoathiri
mazingira.
Mbunge wa Makete, Mhe. Festo
Sanga ameipongeza Serikali kwa kuamua kutekeleza mradi huo ambapo ameeleza
kuwa, toka mchakato wa utekelezaji uanze viongozi na wananchi wa eneo
hilo wamekuwa wakishirikishwa.
Pia ameishukuru Serikali kwa
kazi ya usambazaji umeme wilayani Makete ambapo vijiji vyote 68 vina umeme na
kazi iliyobaki sasa ni kusambaza umeme vitongojini.
Awali, Mratibu wa Mradi huo,
Mhandisi Toto Zedekia alieleza kuwa, mradi unafaida mbalimbali ikiwemo kuchangia
kuwepo kwa umeme wa kutosha na hivyo kuchangia kukua na kuendeleza sekta
ya viwanda nchini na kuongeza pato la taifa kupitia viwanda.
Ameongeza kuwa, Mradi huo
utasaidia kuongeza kiwango cha umeme kwenye gridi ya taifa na kuwepo kwa ajira
zisizo rasmi na ajira rasmi wakati wa ujenzi, pia kuinua hali ya maisha ya
wanachi wa maeneo ya mradi kupitia biashara mbalimbali.
Amesema kuwa, mradi unahusiaha
pia ujenzi wa miundombinu wezeshi kama vile barabara.
Posted by MROKI
On Thursday, February 22, 2024
No comments
0 comments:
Post a Comment