Nafasi Ya Matangazo

February 03, 2024

Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said ameitakaTume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuwa na makongamano ya kuwakutanisha wabunifu waliofanikiwa na wale wachanga ili kuwasaidia hawa wadogo kufikia hatua za kubiasharisha bunifu zao.

Hayo yamesemwa tarehe 02 Februari 2024 na Mhe. Zena Said wakati wa uzinduzi wa kituo mama cha Ubunifu cha iBUA Innovation Hub kilichopo katika Ofisi za COSTECH kisiwani Zanzibar.

Ukumbi huo mama wa Ubunifu umeanzishwa na COSTECH kwa kushirikiana na Tume ya Mipango Zanzibar (ZPC) ambao wote kwa pamoja wana jukumu la kuratibu, kukusanya, kusambaza na kutafsiri matokeo ya tafiti zilizofanyika ili matokeo hayo yasaidie kutatua changamoto za kimaendeleo ya Kiuchumi na kijamii, Alisema.

Alisema kituo hiki mama cha Ubunifu kimeanzishwa kwa mashirikiano baina ya COSTECH na ZPC kupitia makubaliano (MoU) yaliosainiwa mwaka 2023.

Aidha amesema duniani kote masuala ya Ubunifu yamekuwa yakitumika kama nyenzo muhimu ya kuleta Maendeleo ambapo nchi nyingi zilizojikita katika kuhamasisha na kukuza tafiti, Ubunifu na matumizi ya teknolojia zimepiga hatua kubwa ya Maendeleo.

Amefafanua kuwa kituo hiki kitawashirikisha na kuwaunganisha watafiti kutoka Taasisi za Utafiti na Maendeleo, Vyuo Vikuu na wadau wengine katika kufanya kazi kwenye miradi inayolenga kuleta Ubunifu na kukuza teknolojia mpya ili kuchangia ukuaji, uzalishaji na uendelezaji wa teknolojia zinazoleta suluhisho la changamoto zinazoibuliwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt. Amos Nungu amesema Taasisi hiyo inayofuraha kufanikisha kukamilika kwa kituo hiki mama cha Ubunifu kwani kitaendelea kuongeza ufanisi na upatikanaji wa wabunifu kwa upande wa Zanzibar.

Uzinduzi wa iBUA Innovation Hub ni uthibitisho wa dhamira yetu thabiti ya kukuza ubunifu, maendeleo ya kiteknolojia na ukuaji wa uchumi katika visiwa hivi vya Zanzibar.

Amesema, wazo la kuanzisha Ukumbi wa Ubunifu wa iBUA Zanzibar umetokana na mafanikio yaliyopatikana kutoka Buni hub, ambapo imetoa msaada wa kitaaluma kwa Hub zaidi ya 60 nchi nzima, takribani kampuni changa (startups) 50, vijana 150 wamepata mafunzo ya ujasiliamali na kupokea wadau kufanya mikutano yao katika ukumbi huo.

Dkt Nungu amesema, Ukumbi wa Ubunifu wa iBUA unategemea kutoa huduma Kuongeza uwezekano wa wadau kutoa usaidizi kwa wabunifu katika eneo mahususi, kusaidia wabunifu kupata ushauri kutoka eneo la karibu, kujenga na kuvutia tamaduni/tabia ya ubunifu katika jamii, kuongeza ufahamu wa fursa zinazopatikana kwa watafiti na sekta ya biashara, kuongeza uelewa wa maendeleo ya nchi/ulimwengu na jinsi ya kutumia fursa pamoja na upatikanaji wa wataalamu na washikadau kushiriki katika kuendeleza ubunifu.

Kumbi hii ya iBUA sio tu inahusu teknolojia mpya au utafiti; ni kuhusu ujumuishi na kujenga mazingira ambapo maarifa asilia yanakidhi mbinu za kisasa, ambapo wataalamu waliobobea hushirikiana na vijana wenye vipaji, na ambapo kila Mzanzibari, bila kujali hali yake au elimu yake, atapata nafasi ya kuchangia maendeleo yetu ya pamoja.

Tunapozindua Kumbi hii ya Ubunifu, tutafakari juu ya ukubwa wa uhitaji wake kwa hapa Zanzibar na ni nafasi ambapo vijana wetu wanaweza kukuzwa katika mazingira ya ubunifu na wajasiriamali.

Kwa kuthibitisha hili, zaidi ya Hub meneja 25 wanatoka kwenye Hub zisizopungua 22 zilizoko mashuleni, wamehitimu mafunzo katika ukumbi huu.

Posted by MROKI On Saturday, February 03, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo