Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia
Suluhu Hassan amesema serikali za Tanzania na Ujerumani zimekubaliana kuwa na
mazungumzo ya ushirikiano wa maendeleo yatakayofanyika mwaka 2024.
Serikali hizo zimeagiza timu za wataalam kutoka pande
zote mbili kuendelea kuwa na mazungumzo ya mara kwa mara yanayolenga kuimarisha
ushirikiano na kubainisha maeneo mapya yenye umuhimu kwa nchi zote.
Rais Samia amesema hayo leo, wakati akizungumza na
Waandishi wa Habari mara baada ya kumpokea na kuzungumza na Rais wa Jamhuri ya
Shirikisho la Ujerumani, Dkt. Frank Walter Stainmeier ambaye yupo nchini kwa
ziara ya kikazi ya siku tatu.
Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa Tanzania iko tayari
kufungua majadiliano kuhusu yaliyopita kwenye historia ya Utawala wa Ujerumani nchini
ambapo mojawapo ni urejeshaji wa mabaki yaliyopo kwenye makumbusho mbalimbali
za Ujerumani kwa
familia zao.
Rais Samia amesema anatambua juhudi za pamoja zinazofanywa
na taasisi za Serikali hizo mbili
zinazolenga kufanikisha azma hiyo ikiwemo pia kuwajengea uwezo wataalam na
kuongeza uwezo wa makumbusho za Tanzania na Ujerumani.
Rais Samia pia ameishukuru Ujerumani kwa namna
inavyounga mkono Tanzania kwenye miradi ya maendeleo hususan sekta za afya,
maji, kilimo, elimu, utalii, utamaduni, michezo, ulinzi, maliasili, uhifadhi wa
mazingira na udhibiti wa fedha.
Kuhusu uwekezaji, Rais Samia amesema viongozi wote
wawili wamekubaliana na kusisitiza mchango muhimu wa biashara na uwekezaji
katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
familia zao.
0 comments:
Post a Comment