Na Mwandishi maalumu – Dar es-salaam
Wagonjwa 10 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa
moyo wa kuzibua mishipa ya damu iliyoziba katika kambi maalumu ya matibabu ya
moyo ya siku saba.
Kambi hiyo iliyomalizika leo katika Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam imefanywa na madaktari
bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa JKCI kwa kushirikiana na mwenzao
kutoka Hospitali ya Max iliyopo nchini India.
Akizungumzia kambi hiyo Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji
wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema kambi
hiyo imefanyika kwa mara ya nne kwa kushirikiana na wataalam kutoka Hospitali
ya Max kuwafanyia upasuaji wagonjwa waliohitaji utaalam zaidi kutokana na mioyo
yao kuwa na uwezo mdogo wa kufanya kazi.
Dkt. Angela alisema kambi hiyo ililenga kufanya
upasuaji mkubwa wa moyo kwa watu wazima ambao wanamishipa ya moyo iliyoziba
lakini pia viwango vya ufanyaji kazi wa mioyo yao kuwa chini ya asilimia 30.
“Upasuaji ambao tumewafanyia wagonjwa hawa ni mgumu
kidogo, tumekuwa tukiwafanyia uchunguzi wagonjwa hawa na kuwakaribisha wenzetu
kutoka Hospitali ya Max ili kwapamoja tuweze kuwahudumia wagonjwa hawa lakini
pia tuweze kuongeza ujuzi wetu katika kuwahudumia wagonjwa wa aina hii”,
“Katika kambi hii wagonjwa wamepandikizwa mishipa ya
moyo mitatu na wengine zaidi ya mitatu bila ya kuusimamisha moyo kwa mafanikio
makubwa hii kwetu sisi ni hatua kubwa katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo”,
alisema Dkt. Angela
Aidha Dkt. Angela alisema JKCI inategemea kufanya
upasuaji wa mshipa mkubwa wa moyo ambao umetanuka, kubadilisha mishipa ya moyo
pamoja na kuweka mlango mpya kwa wagonjwa ambao wana matatizo ya mishipa
mikubwa ya moyo kutanuka.
Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na
mishipa ya damu kutoka Hospitali ya Max iliyopo nchini India Subhash Sinha
alisema ushirikiano wake na wataalam wa JKCI unaonyesha mafanikio makubwa tangu
walipoanza kushirikiana hadi sasa.
Dkt. Sinha alisema kupitia upasuaji wa moyo ambao
amekuwa akifanya na wataalam wa JKCI amekuwa pia akitoa mafunzo na mbinu
mbalimbali za kufanya upasuaji mkubwa wa mishipa ya moyo kwa wagonjwa ambao
mapigo yao ya moyo yapo chini ya asilimia 30 bila ya kuusimamisha moyo.
“Ujio wangu hapa JKCI kwa kawaidia huwa ni wa wiki
moja, naamini hizi wiki moja moja ninazokuja kuwasaidia wagonjwa kupata
matibabu wataalam wa JKCI nao hupata nafasi ya kujifunza kwani sasa naona
mabadiliko makubwa wakati tunafanya upasuaji”, alisema Dkt. Sinha.
Dkt. Sinha alisema anatamani siku moja JKCI iwe
Taasisi kubwa Afrika inayotegemewa na wagonjwa wa moyo waliopo Afrika kwani
gharama za matibabu ni zakawaida tofauti na zile zinazotolewa nje ya Afrika
lakini pia uwekezaji wa vifaa tiba vilivyopo katika Taasisi hiyo
vinajitosheleza kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.




0 comments:
Post a Comment