Masudi Yasin Kilyamanda (aliyevaa kofia) mkulima wa tumbaku katika Kijiji cha Lufwisi, Kata ya Igigwa Wilayani Sikonge Mkoani Tabora akiwa na Viongozi wa Benki ya Azania baada ya kukabidhiwa ufunguo na namba ya usajili ya trekta lenye thamani ya sh mil 111.7, alilokopeshwa na benki hiyo kwa ajili ya kufanikisha shughuli zake za kilimo cha tumbaku, alizeti na mahindi. /Picha: Lucas Raphael.
*********
Na Lucas Raphael,TaboraKATIKA kuunga mkono juhudi za
serikali ya awamu ya sita za kuboresha shughuli za wakulima nchini, benki ya
Azania imeanza kutoa mikopo ya zana bora za kilimo kwa wakulima wa tumbaku
Mkoani Tabora ili kuwainua kiuchumi.
Akikabidhi mkopo wa trekta kwa
mmoja wa wakulima wa Mkoa huo Masudi Yasin, mkazi wa Kata ya Igigwa, wilayani
Sikonge, kwenye maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD), Waziri wa Kilimo
Hussein Bashe amepongeza benki hiyo kwa kuunga mkono juhudi za serikali kwa
vitendo.
Alibainisha kuwa taasisi za
fedha zina mchango mkubwa sana katika kuboresha shughuli za wakulima na kuinua
maisha yao, hivyo akawahakikishia kuwa serikali itaendelea kuwapa ushirikiano
ili kufanisha utekelezaji majukumu yao.
‘Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa
na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ina nia ya dhati ya kuinua wakulima nchini,
ndiyo maana imetenga bajeti ya kutosha mwaka huu ili kuboresha sekta hii’,
alisema.
Meneja wa Benki hiyo
anayeshughulikia Kilimo Agustin Matutu alisema wamejipanga vizuri kuhudumia
wakulima wote kwa kuwapatia mikopo ya trekta na zana nyingine za kilimo kwa
riba nafuu.
Aliongeza kuwa kwa kutambua
umuhimu wa sekta ya kilimo nchini wataendelea kushirikiana na serikali ili
kuhakikisha malengo yake ya kuinua sekta hiyo yanatimia kwa manufaa ya
wananchi.
Naye Afisa Mahusiano wa Benki
hiyo Denis Sebastian alibainisha kuwa taasisi hiyo ni mdau mkubwa wa wakulima
na wafugaji nchini hivyo wanatoa mikopo hiyo ili kuwasaidia kutimiza malengo
yao.
Alisema mikopo hiyo inatolewa
ndani ya wiki mbili tu na masharti yamerahishwa sana ili kuwezesha wote
wanaoomba zana hizo kuzipata ndani ya muda mfupi ili kuendelea na shughuli zao.
Aliongeza kuwa hadi sasa
wamepokea zaidi ya maombi 15 ya mikopo ya zana hizo na kuwahakikishia kuwa wote
watapatiwa huku akitoa wito kwa wakulima wote wanaohitaji kuwezeshwa mikopo
hiyo kupeleka maombi yao.
Akitoa neno la shukrani baada
ya kukabidhiwa ufunguo na namba ya usajili ya trekta hilo, mkulima Masudi Yasin
alipongeza benki hiyo kwa kumwezesha chombo hicho chenye thamani ya sh mil
111.7 na kubainisha kuwa alikuwa anakihitaji kwa muda mrefu sana.
Alifafanua kuwa awali alikuwa
anashindwa kupata mavuno mengi kutokana na zana duni alizokuwa akitumia lakini
sasa ana uhakika wa kulima ekari zaidi ya 94 na kuvuna zaidi ya kilo 53,000 za
mazao ya alizeti, tumbaku na mahindi.







0 comments:
Post a Comment