Wizara
ya Ujenzi na Uchukuzi imeliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kuidhinisha zaidi ya shilingi Trilioni 3.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
ya miundombinu ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege, reli, meli, vivuko, majengo
ya Serikali na ununuzi wa ndege.
Fedha
hizo zimeombwa ili kui marisha huduma za usafiri na usafirishaji kote nchini na
hivyo kuimarisha ukuaji wa uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa
ujumla.
Akiwasilisha
mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2023/2024
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema pamoja na mambo
mengine fedha hizo zinatarajiwa kujenga miradi ya kihistoria yenye urefu wa
kilometa 2,035 nchini ikiwemo barabara za Kidatu - Ifakara - Lupilo - Malinyi -
Kilosa kwa Mpepo - Londo - Lumecha hadi Songea KM 435.
Miradi
mingine ni barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti River – Lalago - Maswa
hadi simiyu KM 339 na barabara ya Handeni – Kibirashi – Kijungu – Kibaya –
Njoro – Olboroti – Mrijochini – Dalai – Chambalo – Chemba – Kwa mtoro hadi
Singida KM 460.
Aidha,
Prof. Mbarawa amefafanua kuwa Serikali itaendeleza ujenzi wa reli ya kisasa
(SGR) kutoka Dar es Salaam – Mwanza KM 1,219 katika vipande vitano vya awamu ya
kwanza ya ujenzi ili kuhakikisha vinakamilika kwa wakati na kwa thamani halisi
ya fedha.
“Mheshimiwa
Spika vipande hivyo ni Dar es Salaam – Morogoro KM 300, Morogoro – Makutupora
KM 422, Mwanza – Isaka KM 341,
Makutupora – Tabora KM 368 na Tabora – Isaka KM 165 ambavyo ujenzi wake
uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha,
Serikali itaendelea na awamu ya pili ya ujenzi wa SGR sehemu ya Tabora – Kigoma
KM 506 ambapo mkataba wake umesainiwa na kwa sasa mkandarasi anakamilisha
maandalizi ya ujenzi.
Awali
akitaja vipaumbele vya Sekta ya Ujenzi Prof. Mbarawa amesema ni pamoja na kuanza
ujenzi wa barabara ya Express way
kutoka Kibaha-Chalinze-Morogoro yenye urefu wa KM 205 kwa mfumo wa PPP na kuendeleza ujenzi wa barabara kuu zenye urefu wa KM 350
ambapo kilometa 282 zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na kilometa 68
ni miradi mipya.
“Wizara
imepanga kufanya matengenezo ya kilometa 38,384.90 za barabara kuu na barabara
za mikoa pamoja na matengenezo ya madaraja 3,129”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Kuhusu
vipaumbele vya Sekta ya Uchukuzi, Prof. Mbarawa ameeleza kuwa Serikali inakusudia
kutekeleza miradi ya miundombinu ya reli ambapo ujenzi wa reli mpya ya SGR na
ukarabati wa reli ya zamani ya MGR na TAZARA.
Waziri Mbarawa amesema katika kuimarisha bandari
nchini Serikali imepanga kuboresha bandari zilizomo katika maziwa makuu ikiwemo
bandari ya Bukoba, Kemondo bay, Mwanza South, Mwanza North, Kibirizi na Ujiji.
Serikali itaendelea na ununuzi wa mitambo ya kuongozea
ndege na uendelezaji wa Chuo cha mafunzo ya usafiri wa anga ikiwa ni pamoja na
mradi wa ununuzi wa rada mpya, na vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya hali ya
hewa.
Kati ya zaidi ya shilingi Trilioni 3.5 zinazoombwa katika
bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu takriban
shilingi Trilioni 1.5 ni kwa ajili ya Sekta ya Ujenzi na shilingi Trilioni 2.086
kwa ajili ya Sekta ya Uchukuzi.
Imetolewa na kitengo cha habari na mawasiliano
Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi




0 comments:
Post a Comment