Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng.
Godfrey Kasekenya, akihutubia wananchi wakati wa utiaji saini mkataba wa ujenzi
wa barabara ya Sengerema - Nyehunge (km 54.4) kwa kiwango cha lami na ujenzi wa
Kivuko kipya cha Buyagu – Mbalika, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Ufundi na Umeme (TEMESA), Bw. Lazaro Kilahala na Meneja wa Kampuni Songoro
Marine, Major Songoro wakionesha mkataba wa ujenzi wa kivuko kipya cha Buyagu –
Mbaika mara baada ya kutiliana saini kitakachogharimu kiasi cha Bil 3.8
wilayani Sengerema mkoani Mwanza. Kivuko hicho kipya kitakuwa na uwezo wa kubeba
uzito wa tani 50 ikijumuisha abiria 100 (waliokaa 50 na waliosimama 50) pamoja
na magari madogo 6.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Barabara (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila, akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara
ya Sengerema - Nyehunge (km 54.4) kwa kiwango cha lami wakati wa utiaji saini
wa mkataba huo na Mwakilishi kutoka kampuni ya AVM - Dilingham kwa gharama
takribani Bilioni 73. mkoani Mwanza. Barabara hiyo ni sehemu ya mtandao wa
barabara inayounganisha Mkoa wa Mwanza na Mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Ufundi na Umeme (TEMESA), Bw. Lazaro Kilahala, akitoa taarifa ya ujenzi wa
kivuko kipya kitachotoa huduma kati ya Buyagu – Mbalika, mkoani Mwanza. Kivuko
hicho kitakuwa na uwezo wa kubeba uzito wa tani 50 ikijumuisha abiria 100 (waliokaa
50 na waliosimama 50) pamoja na magari madogo 6.
Wananchi wakifatilia hotuba ya
mgeni rasmi Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, wakati wa utiaji
saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Sengerema - Nyehunge (km 54.4) kwa
kiwango cha lami na ujenzi wa Kivuko kipya cha Buyagu – Mbalika, wilayani
Sengerema, mkoani Mwanza.
Mkataba wa barabara umesainiwa
kati ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), na kampuni ya AVM - Dilingham
ya Uturuki kwa gharama ya shilingi Bilioni 73 na mkataba wa kivuko kipya
umesainiwa kati ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na kampuni ya Songoro
Marine kwa gharama ya Bilioni 3.8.
Akishuhudia utiaji saini
mikataba hiyo mkoani humo, Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya,
amesema kuwa miradi hiyo itakapokamilika itaimarisha shughuli za kiuchumi kwa
wananchi waishio maeneo ya Wilaya ya Sengerema hasa Halmashauri ya Buchosa.
Aidha, amesema miradi hiyo
itasaidia kutengeneza ajira kwa wananchi wa Wilaya hiiyo wakati wa utekelezaji
wa ujenzi.
Eng. Kasekenya ameziagiza
TANROADS na TEMESA kuisimamia vyema miradi yote hiyo ili thamani ya fedha ipatikane
na kukamilika kwa wakati.
Ameeleza kuwa ujenzi wa
barabara na kivuko hicho utatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani kwa asilimia
100 ikiwa ni moja ya juhudi na mikakati ya Serikali chini ya Uongozi thabiti wa
Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuboresha maisha ya wananchi
wake hususan wana Sengerema.
Akiongelea kuhusu barabara
Eng. Kasekenya ameeleza kuwa barabara hiyo ni sehemu ya mtandao wa barabara
muhimu za nchi yetu ambayo inaunganisha Mkoa wa Mwanza na Mikoa ya Geita,
Kagera na Kigoma.
"Barabara hii
itakapokamilika itachochea shughuli za kiuchumi kama vile usafirishaji wa
bidhaa mbalimbali na abiria, bidhaa za uvuvi, mazao ya chakula, mazao ya
biashara mazao ya misitu na shughuli za kijamii kwa ujumla", amesema Eng.
Kasekenya.
Eng. Kasekenya ametaja miradi
mingine ya madaraja na barabara ambayo ujenzi/ukarabati wake unaendelea kwa
kugharamiwa na Serikali ni ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu (mita
3,000) pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa km 1.66, barabara ya Tarime
– Mugumu, sehemu ya Tarime hadi Nyamwaga (km 25), barabara ya Bugene hadi
Burigi Chato National Park (km 60), Daraja la Kitengule lenye urefu wa mita 140
pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa km 18, barabara ya Nyamuswa - Bunda
- Kisorya hadi Nansio sehemu ya Nyamuswa – Bunda hadi Bulamba (km 56.4), na
barabara ya Makutano – Nyamuswa hadi Ikoma Gate sehemu ya Sanzate hadi Natta
(km 40).
Kwa upande wa ujenzi wa kivuko
kipya Eng. Kasekenya amesema kuwa kivuko hicho kitatoa huduma Buyagu na Mbalika
katika Wilaya ya Sengerema na Misungwi lengo likiwa ni kuwapatia usafiri ulio
salama na wenye uhakika wananchi wa maeneo hayo ambayo wamekuwa wakitumia
mitumbwi kwenye eneo hilo lenye umbali wa takribani kilometa saba.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu
wa TANROADS, Eng. Rogatus Mativila, amesema kuwa zabuni za ujenzi wa barabara
hiyo zilitangazwa tarehe 13 Juni, 2022 na kufunguliwa tarehe 30 Agosti, 2022
ambapo jumla ya zabuni12 zilipokelewa na kufanyiwa tathmini na Mkandarasi
aliyeshinda tuzo ni Kampuni ya AVM-Dilingham Construction International Inc. ya
nchini Uturuki kwa muda wa miezi 28.
Naye Mtendaji Mkuu wa TEMESA,
Lazaro Kilahala, amesema kuwa kivuko kipya cha Buyagu - Mbalika baada ya ujenzi
kukamilika kitakuwa na uwezo wa kubeba uzito wa tani 50 zikijumuisha; abiria
100 (waliokaa 50 na waliosimama 50) pamoja na magari madogo 6.
Kilahala ameongeza kuwa mbali
na ujenzi wa kivuko hicho wanaendelea na utekelezaji wa vivuko vingine ambapo
jumla ya miradi mitano ya ujenzi wa vivuko vipya, miradi 18 ya ukarabati wa
vivuko na miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vivuko
imekwishasainiwa na inatekelezwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 60.72.
Miradi hiyo iliyosainiwa ni
moja ya mkakati wa Serikali ya kuwaondolea wananchi kero ya usafiri wa kivuko
na kuboresha mtandao wa barabara na madaraja ili kuongeza ufanisi katika sekta
ya usafiri na usafirishaji hapa nchini.




0 comments:
Post a Comment