Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekutana na kuzungumza na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Andrew Lentz, Ikulu Chamwino, Dodoma.
Miongoni wa masuala waliyojadili ni kukuza maeneo muhimu ya ushirikiano baina ya
Tanzania na Marekani na kuthibitisha dhamira ya pamoja ya kuendeleza ushirikiano wa
kisasa wenye manufaa kwa mataifa yote mawili.
Kaimu Balozi Lentz, aliyeambatana na Mshauri wa Masuala ya Kisiasa na Uchumi wa
ubalozi huo, Bw. Andrew Howard alisisitiza nia ya Marekani kuimarisha mahusiano na
ushirikiano katika masusla ya kiuchumi, kisiasa na kiusalama kati ya Tanzania na
Marekani, akisisitiza kuwa dhamira ya Marekani ni kushirikiana na Tanzania kwa misingi
ya ustawi wa pamoja, sio utegemezi wa misaada.
Mazungumzo hayo yalijikita katika kupitia hatua za majadiliano ya miradi mikubwa ya
kimkakati inayoihusisha Marekani nchini.
Pande zote mbili zilikubaliana kumalizia mazungumzo ambayo yako hatua za mwisho,
ikiwemo Mradi wa LNG na Mradi wa Tembo Nickel, kabla ya kutiwa saini rasmi hivi
karibuni, pamoja na Mradi wa Mahenge Graphite ulioko katika hatua za maandalizi.
Rais Samia alikaribisha na kuunga mkono dhamira ya Marekani na kuthibitisha kuwa
Tanzania inaendelea kukamilisha taratibu za uwekezaji zilizosalia.
“Kama taifa lisilofungamana na upande wowote, Tanzania iko wazi na tayari kushirikiana
na washirika wote wanaoheshimu uhuru na kuthamini maono yetu ya ustawi,” alisema
Rais Samia.
“Miradi hii ya kimkakati ina umuhimu mkubwa kwa taifa, na tumejidhatiti kuikamilisha ili
kufungua ajira, kuimarisha uwekezaji na kuongeza ustawi wa wananchi wetu.”
Rais Samia pia alibainisha kuwa zaidi ya kampuni 400 kutoka Marekani zinafanya kazi
nchini, suala linaloashiria uwepo wa mazingira thabiti ya uwekezaji na uhusiano wa muda
mrefu wa kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.
Mbali na sekta za uwekezaji, mazungumzo yao yaligusia maeneo mengine mapana ya
ushirikiano yakiwemo masuala ya utengamano wa kisiasa, usalama wa kikanda, mageuzi
ya kiuchumi, ukuaji wa sekta binafsi, ushirikiano katika sekta ya afya na fursa za
kubadilishana uzoefu kati ya wananchi wa Tanzania na Marekani.
Kaimu Balozi Lentz alimpongeza Rais Samia kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na
kueleza utayari wa Serikali ya Marekani kuunga mkono utekelezaji wa Dira hiyo pamoja
na falsafa ya 4R inayolenga kuboresha misingi ya demokrasia na utawala bora.
Kwa pamoja, nchi zote mbili zilikubaliana kuwa mawasiliano thabiti, ushirikiano endelevu
na utekelezaji wa wakati wa makubaliano yaliyosalia ni msingi muhimu wa kufungua fursa
kamili za mahusiano ya Tanzania na Marekani.
Taarifa Zaidi
Mkutano huu ni hatua muhimu katika kufungua ukurasa mpya wa uhusiano kati ya
Marekani na Tanzania.
Dhamira iliyooneshwa na serikali zote mbili inaashiria mwanzo mpya wa uhusiano wa
uwazi unaochagizwa na sekta binafsi na unaolenga ustawi wa pamoja, kuheshimiana na
ushirikiano wa kimkakati wa muda mrefu.
Miradi Mikubwa ya Kimkakati
1. Mradi wa Gesi Asilia (LNG) — Thamani inayokadiriwa: USD bilioni 42
Mradi mkubwa wa maendeleo ya gesi asilia unaohusisha kampuni za kimataifa za
nishati wenye lengo la kuchochea matumizi ya rasilimali gesi katika ukanda wa
bahari kuu.
Kukamilika kwake kunatarajiwa kuongeza mapato ya nchi, kuzalisha
maelfu ya ajira na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa
LNG duniani.
2. Mradi wa Tembo Nickel — Thamani: USD milioni 942
Uwekezaji muhimu katika madini ya nikeli yaliyopo Ngara, ambayo ni madini
muhimu katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme. Mradi huu utachochea
kasi ya uchumi wa viwanda, kuimarisha mnyororo wa thamani wa nishati safi
duniani na kuongeza mapato ya Tanzania yatokanayo na mauzo ya nje.
3. Mradi wa Mahenge Graphite — Thamani: USD milioni 300
Mradi huu ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya uzalishaji madini ya grafiti
(graphite) yenye ubora wa kiwango cha juu duniani kwa ajili ya kukuza sekta ya
nishati jadidifu. Mradi huu utaiweka Tanzania katika nafasi ya mzalishaji mkuu
wa madini haya.


.jpeg)



0 comments:
Post a Comment