MKOA wa Dar es Salaam umeandikisha watoto 28,508 wa madarasa ya awali ambayo ni sawa na asilimia 60 ya uandikishwaji kwa mwaka 2023.
Hayo yamesemwa na Ofisa Elimu Mkoa wa Dar Es Salaam, Mwalimu Abdul Maulid ambapo amesema kuwa, mkakati ni kuandikisha watoto 46,000 hadi ifikapo Machi 30, Mwaka huu ambao ni muda wa kufungua zoezi la uandikishwaji.
Amesema kuwa, watoto walioandikishwa ni kuanzia umri wa miaka mitatu hadi mitano ambao wanawaandaa kujiunga na darasa la kwanza mara baada ya kufikisha umri wa miaka sita na kuendelea.
Amesema kuwa, katika zoezi hilo wameweza kuandikisha watoto 53 wenye ulemavu, kati yao wavulana 33 na wasichana 20, hivyo basi wanaweza kuongezeka kutokana na bado kuwepo Kwa muda wa uandikishwaji.
" Mwaka huu mkakati wetu ni kuandikisha watoto 46,000 ili waweze kujiunga na madarasa la awali, hivyo basi tunaamini idadi hiyo inaweza kuongezeka," amesema Mwalimu Maulid.
Ameongeza kuwa, licha ya kuongezeka kwa watoto hao, serikali imeweka kipaumbele cha kuongeza idadi ya walimu wenye sifa ambao watafundisha kwenye madarasa hayo.
" Tumeanza kujenga madarasa yanayozungumza katika baadhi ya shule, lengo ni kuwavutia watoto wetu kwa sababu ni wadogo sana na wanapenda kucheza waweze kusoma katika mazingira bora na rafiki," amesema.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dar Es Salaam, Nyamala Elisha amesema kuwa, serikali itaendelea kushirikiana na wazazi ili kuhakikisha watoto wanasoma katika mazingira salama.
" Mtoto mdogo anahitaji ulinzi na upendo ili aweze kusoma katika mazingira rafiki na salama, ni jukumu letu kushirikiana wazazi, walezi na jamii kwa ujumla ili kutoa elimu na kuhakikisha mtoto anapotoka nyumbani kwenda shule analindwa, na anaporudi analindwa,"amesema Nyamala.
Ameongeza kuwa, watoto wanaotumia mabasi ya shule kwenda na kurudi wanapaswa kuwalinda watoto hadi wanapofika nyumbani ili kuepusha na hatari zozote ambazo wanaweza kukumbana nazo.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk. John Kalaghe amesema kuwa, licha ya kuwepo kwa ongezeko la watoto wanaoanza madarasa la awali, lakini kuna changamoto ya walimu, vitendea kazi pamoja na miundombinu.
" Kuna idadi ndogo ya walimu wenye sifa ambao wanapaswa kufundisha madarasa la awali, kwa sababu hawa watoto ni wadogo na wanahitaji ulinzi wa hali ya juu kuanzia shuleni hadi nyumbani, hivyo basi ikiwa Serikali inaongezeka madarasa ongezeko hilo liende sambamba na walimu, vitendea kazi na miundombinu wezeshi," amesema Dk. Kalaghe.
Kwa upande wake, mzazi Amina Juma (33) ameishauri serikali kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwalinda watoto.
" Watoto wanaoanza madarasa ya awali ni wadogo, wanahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wazazi, walimu na jamii kwa ujumla, hivyo basi tunapaswa kushirikiana kwa pamoja ili kuwalinda kuanzia wanapotoka nyumbani kwenda shule hadi wanaporudi," amesema Amina.
Ameongeza kuwa, elimu itolewe kwa jamii Ili kila mmoja aone ni jukumu lake kumlinda mtoto hata kama sio wake, jambo ambalo linaweza kukomesha vitendo vinatohatarisha usalama wa mtoto.
Serikali inatekeleza Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ya mwaka 2021/26 ambayo imelenga kuongeza kasi ya mafanikio yanayopatikana katika huduma za MMMAM ambazo ni pamoja na afya Bora, elimu, Malezi yenye mwitikio, lishe, ulinzi na usalama.
Programu hiyo itasaidia kuboresha uratibu wa huduma kwa kuimarisha utekelezaji wa Sheria na Sera zinazohusu masuala ya MMMAM, Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2008, Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya Mwaka 2008, Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Sera ya Afya ya Mwaka 2007 ambazo kwa pamoja zinashughulikia mahitaji ya mtoto kuanzia umri sifuri hadi miaka minane.





0 comments:
Post a Comment