Meneja
wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Tabora Mjini,
Mhandisi Subira Manyanya akitoa taarifa ya mipango ya utekelezaji miradi ya
barabara katika kata zote wilayani humo juzi katika kikao cha madiwani. ***********
Na Lucas Raphael,Tabora
WAKALA wa Barabara za Vijijini
na Mijini (TARURA) katika Wilaya ya Tabora anatarajia kutengeneza mtandao wa
barabara zenye urefu wa km 100.03 katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Hayo yamebainishwa na Meneja
wa Wakala huo Wilaya ya Tabora Manispaa Mhandisi Subira Manyama alipokuwa
akitoa taarifa katika kikao cha baraza la madiwani jana.
Alisema katika mwaka wa fedha
2023/2024 wanatarajia kuzifanyia matengenezo barabara za Vijijini na Mijini
zenye urefu wa km 100.03 ikiwemo ujenzi wa makalvati 29, vivuko 20 na mifrereji
3620.
Alifafanua kuwa jumla ya sh
bil 2.3 zinatarajiwa kutumika katika mpango wa utekelezaji matengenezo hayo,
fedha za bajeti hiyo zitahusisha zile za Mfuko wa Barabara (Road Fund), Jimbo
na Tozo ya Mafuta.
Alibainisha kuwa katika bajeti
hiyo fedha kutoka Mfuko wa Barabara (Road Fund) kiasi cha sh bil 1.3
zinatarajiwa kutumika kwa matengenezo ya
kawaida ya barabara zenye urefu wa km 83.32 kwa gharama ya sh mil 319.3
Kazi nyingine ni matengenezo
ya barabara korofi zenye urefu wa km 7.54 zitakazogharimu mil 67.8, matengenezo
ya muda maalumu ya barabara zenye urefu wa km 9.7 kwa gharama ya sh mil 185.4,
ujenzi wa makalvati 29, boksi kalvati 3, mifereji mita 3620 na vivuko kwa
gharama ya sh mil 644.5.
Kiasi cha sh mil 86.2 za mfuko
huo kinatarajiwa kutumika kwa ajili ya usimamizi wa matengenezo ya barabara
hizo na ujenzi wa makalvati na kiasi cha sh mil 500 za tozo za mafuta
kikitarajiwa kutumika kwenye ujenzi wa barabara ya Nyerere (Kidongo Chekundu)
yenye urefu wa km 0.8, ya Viseko km 3.22 na Mwilu km 0.5.
Mhandisi Manyama alibainisha
kuwa katika bajeti hiyo wanatarajia kujenga barabara ya Warangi yenye urefu wa
km 1 kwa kiwango cha lami kwa gharama ya sh mil 500 za Mfuko wa Jimbo.
Alifafanua kuwa Wilaya hiyo ina Mtandao wa
barabara wenye jumla ya km 775.6 ambapo km 481.3 ni za mjazio (feeder roads) na
km 294.3 ni za mkusanyo (collector roads) na kubainisha kuwa hadi sasa barabara
za lami ni km 54.34, za changarawe km
88.6 na za udongo km 633.15.
Posted by MROKI
On Tuesday, January 10, 2023
No comments
0 comments:
Post a Comment