Nafasi Ya Matangazo

January 10, 2023

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Ramadhan Shaban Kapela, ambaye pia ni diwani wa kata ya Isevya, akiongoza kikao cha baraza la madiwani wa manispaa hiyo juzi katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo, aliyeketi kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Seif Salumu na kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini Eamanuel Adamson Mwakasaka. 
********** 
Na Lucas Raphael,Tabora
Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini Emanuel Adamson Mwakasaka alimshukuru Rais kwa kuwaongezea bajeti Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) hali iliyopelekea barabara na madaraja kutengenezwa katika kata zote.
 
Wakiongea kwa nyakati tofauti katika kikao cha bajeti cha baraza hilo kilichofanyika juzi katika ukumbi wa mikutano wa manispaa hiyo walisema serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Samia imewatendea haki wananchi.
 
 Mwakasaka alisema kwamba serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA)imefanikiwa kupata fedha za kutosha za kuhakikisha barabara za manispaa hiyo zinapitika muda wote wa mwaka.
 
Ili miundombinu hiyo idumu alishauri watendaji wa vijiji na kata kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi kuhakikisha magari yenye uzito mkubwa hayapitishwi katika madaraja na barabara hizo na ikibidi ziwekwe alama za uzito wa magari.
 
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ramadhan Kapela alisema kwamba madiwani wa halmashauri ya manispaa Tabora wanampongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kasi kubwa ya utekelezaji miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
 
 Alibainisha kuwa miradi mingi katika manispaa hiyo ilikuwa inasuasua kutokana na ufinyu wa bajeti lakini baada ya kuingia madarakani Rais amemwaga fedha katika sekta zote ikiwemo elimu, afya, barabara, maji na nyinginezo hivyo kuongeza kasi ya utekelezaji miradi ya maendeleo katika sekta hizo.
 
Ramadhan alisema Rais Samia kila siku anafanya jambo jipya linalogusa maisha ya wananchi hali inayopelekea kutatuliwa kero zao.
 
Aliongeza kuwa halmashauri hiyo haijawahi kupata asilimia 100 ya makadirio ya bajeti yake ya maendeleo lakini chini ya uongozi wa Rais Samia wameletewa fedha zote walizoomba na kufanikisha utekelezaji mipango yao ya maendeleo.
 
‘Tunamkushukuru sana Rais kwa kutuletea zaidi ya bil 1.5 za ujenzi wa hospitali ya wilaya huduma sasa zinatolewa, pia sh bil 1 kwa ajili ya jengo la utawala na kila mwezi anatuletea fedha za mfuko wa Jimbo na za matumizi mengineyo’, alisema Ramadhan.
 
Aidha alipongeza hatua ya Rais Samia kuanza kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima kwa kuwapunguzia gharama kutoka sh 140,000 hadi sh 70,000 tu kwa mfuko wa mbolea na kubainisha kuwa itawasaidia kuongeza uzalishaji mazao yao.
 
Kaimu Mkurugenzi wa manispaa hiyo Seif Salumu alisema wataendelea kusimamia utekelezaji miradi yote kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha thamani ya fedha (value for money) inaonekana ili kuwanufaisha wananchi.

Posted by MROKI On Tuesday, January 10, 2023 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo