KITUO cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele kilichopo mkoani Mtwara kinachojishughulisha na majukumu ya kufanya utafiti wa mazao makubwa kitaifa ya korosho na mbegu za mafuta ambayo ndani yake kuna ufuta na karanga kimetekeleza agizo la Waziri wa Kilimo kwa kumpeleka Mtaalam wa Kilimo Bora cha zao la Korosho wilayani Manyoni mkoani Singida ili kuwasaidia wakulima.
Akizungumza katika hafla fupi ya kumpokea mtaalam huyo aitwaye George Lucas iliyofanyika ofisi
ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni mkoani hapa jana, Mratibu wa Utafiti wa zao la Korosho Kitaifa kutoka Kituo
cha Utafiti wa Kilimo TARI, Naliendele, Dk. Geradina Mzena alisema wao kama Taasisi
wametekeleza agizo la Waziri wa Kilimo Hussein Bashe la kuwataka kumpeleka
mtaalam wa zao hilo wilayani humo ili kwenda kuwasaidia wakulima wa zao hilo.
"Tumetekeleza agizo la Waziri la kumleta wilayani hapa mtaalam huyu ambaye
atakuwa akiwasidia wakulima ili waweze kulima kilimo cha zao la korosho chenye
tija kwa kutoa mafunzo kwa maafisa ugani na wakulima na si kwa Manyoni pekee
bali na kwa wakulima wa mikoa mingine ya jirani" alisema Dk.Mzena.
Dk.Mzena alisema lengo la TARI nikuona wakulima wanalima kilimo chenye tija
cha zao hilo na wananufaika nacho na wanainuka kiuchumi na Serikali inapata
mapato.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Melkzedeki Humbe
aliishukuru Serikali na TARI kwa hatua hiyo ya kumpeleka mtaalam huyo ambaye
walikuwa wakimuhitaji kwa siku nyingi kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa zao
hilo wilayani humo.
"Tunashukuru sana kwa ujio wa mtalaam wa zao la korosho tunaamini
atasaidia kuinua kilimo cha korosho wilayani kwetu na ujio wake ni neema kwetu
ukizingatia kuwa zao la korosho ni la kimkakati na tegemeo kwa kuinua uchumi wa
wilaya yetu na Taifa kwa ujumla na tutampa ushiriano mkubwa" alisema
Humbe.
Hafla ya kumpokea mtaalaam huyo ilihudhuriwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Rahabu Mwagisa, wataalamu wa kilimo wilayani humo akiwepo na Kaimu Meneja wa Bodi ya Korosho Wilaya ya Manyoni, Ray Mtangi.
0 comments:
Post a Comment