Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) wakikabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa Mlezi wa Kituo cha kulelea watoto yatima na wasiojiweza cha Mtakatifu Theresa, Sister Dinner, Kituo hicho kipo katika Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Tabora ambapo walikabidhi msaada wa vyakula, mafuta, sabuni na vingine vingi jana.
*************
Na Lucas Raphael, TaboraVIONGOZI wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC) wametembelea watoto na wazee wasiojiweza wanaolelewa katika Kituo cha Mtakatifu Theresa cha Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Tabora na Kituo cha Amani maarufu kama Kambi ya Wazee kilichopo eneo la Ipuli mjini Tabora na kutoa misaada mbalimbali.
Misaada iliyotolewa katika Vituo hivyo ni mchele kilo 100, unga kilo 50, sukari kilo 25, maharage kilo 50, mafuta ya kupikia lita 10, mafuta ya kupaka boksi 2, sabuni ya unga ndoo 2, dawa ya meno boksi 2, juisi katoni 4, biskuti boksi 2, pipi mifuko 2, chumvi paketi 20, miswaki mifuko 4 na miche 8 ya sabuni.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya takribani sh mil 1, Mtendaji Mkuu wa Shirikisho hilo Alex Ndihile alisema wametoa msaada huo ili kuonesha jinsi Ushirika unavyojali jamii.
Aliongeza kuwa jamii ni sehemu ya ushirika hivyo msaada huo utasaidia kupunguza changamoto walizonazo katika vituo hivyo hususani mahitaji ya chakula, sabuni za kufanyia usafi, dawa ya meno, vinywaji, mafuta ya kupikia na ya kupaka.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho hilo Silvia Thomas alisema wameguswa kutembelea watoto na wazee hao na kuwapatia misaada ya kibinadamu ili kuonesha upendo wao kwa jamii.
Aliomba taasisi, mashirika na wadau wengine kuendelea kusaidia jamii yenye uhitaji ili kuwawezesha kupata mahitaji yao ya kila siku.
Akitoa neno la shukrani Mlezi wa watoto wanaolelewa katika Kituo cha Mtakatifu Theresa Sister Dinner alisema msaada huo kwa watoto yatima ni sadaka nzuri sana inayopendeza Mungu.
Aliomba Mwenyezi Mungu awape baraka tele ili siku nyingine wawakumbuke tena na kuwaletea msaada wa chakula ikiwemo vifaa vya darasani na kuongeza kuwa msaada huo ni muhimu sana kwa ustawi na afya za watoto hao.
Mwenyekiti wa Kituo cha Kulelea Wazee cha Amani, George Busambilo aliwashukuru Viongozi hao na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee kuwabariki zaidi na kufanikiwa katika mipango yao yote.
Naye balozi wa Kituo hicho Adriano Nduluma aliwaomba waendelee kuwasaidia kwa kuwa hawana uwezo wa kujikimu kwa mahitaji yao ya kila siku na kuongeza kuwa bado wanauhitaji mkubwa wa chakula katika kituo hicho.
Alisema kambi hiyo ina jumla ya wazee wasiojiweza 34 ambapo wanawake ni 9 na wanaume 15 ambao wanaendelea kutunzwa katika kambi hiyo.
0 comments:
Post a Comment